Simba SC imeanza mchakato wa tathmini ya mipango ya ujenzi wa uwanja wake mpya, huku mjadala mkubwa ukiendelea ndani ya klabu kuhusu eneo sahihi la mradi huo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Crescentius Magori, amesema bodi imepokea maoni tofauti kutoka kwa wanachama na wadau kuhusu mahali ambapo uwanja huo unapaswa kujengwa.
Simba ina eneo lake la Bunju nje kidogo ya Dar es Salaam ambalo kwa sasa linatumika kama viwanja vya mazoezi, na ambalo lilikuwa likipendekezwa awali kuwa sehemu ya ujenzi wa uwanja mkubwa wa klabu.
Hata hivyo, amesema mjadala umeibuka kutokana na umbali wa eneo hilo, ambapo baadhi ya wadau wanapendekeza uwanja ujengwe sehemu nyingine iliyo karibu zaidi na makazi ya mashabiki ili kurahisisha ufikikaji, huku Bunju ikiendelea kutumika kama kituo cha mazoezi.
Magori amesema bodi itachambua maoni yote kupitia vikao vyake kabla ya kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu mwelekeo wa mradi huo mkubwa unaosubiriwa kwa muda mrefu na mashabiki wa klabu hiyo.
Ameongeza kuwa kwa sasa hakuna ujenzi wa uwanja mkubwa unaoendelea Bunju zaidi ya maboresho ya kawaida ya miundombinu ya mazoezi.
Akizungumza kuhusu mjadala huo, Magori alisema:
“Kuna mawazo tofauti kuhusu matumizi ya Bunju. Je, tukijenga uwanja pale, watu watafika wakiwa na urahisi? Mashabiki wengine wa Simba wapo Mbagala; umbali hadi Bunju ni mkubwa. Je, wataweza kufika? Mitazamo hii itajadiliwa na Bodi ya klabu kabla ya kufanya maamuzi.”
“Bodi itayachambua yote na kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu eneo ambalo uwanja mpya utajengwa, huku ikizingatia maslahi ya mashabiki na klabu. Wakati ukifika, tutawatangazia kila kitu.”
“Bado hatujapokea taarifa ya mtu anayetaka kujenga uwanja Bunju. Kuna maboresho yanaendelea mara kwa mara. Bodi itakutana kuamua kwa sababu kuna mawazo mbalimbali,” alisema Magori.
Ni wazi baada ya watani zao Yanga kutangaza mchakato wa kujenga uwanja eneo la Jangwani, Simba nayo inajipanga na pengine kutafuta eneo karibu ambalo litawapa urahisi mashabiki wake kuhudhuria mechi.



