Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba SC, Ahmed Ali, amesema klabu hiyo imepokea kwa utulivu mabadiliko ya muda wa mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City, huku akisisitiza kuwa Wekundu wa Msimbazi wako tayari kucheza muda wowote uliopangwa na waandaaji wa ligi.
Mchezo huo, ambao awali ulipangwa kuchezwa saa 10 jioni, sasa utapigwa saa 8 mchana Juni 17 katika Uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya kufuatia mabadiliko yaliyofanywa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania.
Mabadiliko hayo yameibua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki na wadau wa soka mitandaoni, wengi wakijadili ratiba hiyo ya kucheza mchana kuihusu Simba pekee huku vigogo wengine Yanga na Azam Fc wakicheza mechi zao katika muda wa jioni na usiku. Hata hivyo, Simba SC imeweka wazi kuwa haina wasiwasi wowote kuhusu ratiba hiyo mpya.
Akizungumza kuhusu suala hilo, Ahmed alisema klabu imekubaliana na maamuzi ya viongozi wa ligi na itaingia uwanjani kama ilivyopangwa bila malalamiko yoyote.
“Tumepokea kwa moyo mnyoofu mabadiliko ya muda wa mchezo wetu dhidi ya Mbeya City kuwa saa 8 mchana,” alisema Ahmed.
Aliongeza kuwa Simba inaheshimu kanuni na maamuzi ya Bodi ya Ligi, na hivyo haina sababu ya kupinga ratiba hiyo mpya iliyotolewa.
“Tunafahamu mabadiliko hayo yamezingatia kanuni za ligi na sisi tunaheshimu kanuni. Sisi hatuna mashaka na hatuna cha kuhoji kwa sababu ni sehemu ya taratibu za ligi,” alifafanua.
Huu utakuwa mchezo wa kwanza kwa Simba kucheza saa 8 mchana katika msimu huu, ingawa si mara yao ya kwanza kukutana na ratiba kama hiyo katika historia ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba ilirejea mazoezini jana kuanza maandalizi ya mechi za kuhitimisha msimu ambao kabla ya kuelekea mkoani Mbeya, Juni 14 watakuwa dimba la KMC Complex kuikabili Pamba Jiji.



