Kiungo mkabaji wa Uganda, Khalid Aucho, ameanza kuhusishwa tena na uwezekano wa kurejea katika klabu ya Young Africans SC baada ya taarifa kueleza kuwa mkataba wake na Singida Black Stars unafikia tamati mwishoni mwa msimu huu.
Aucho ambaye alisaini mkataba wa mwaka mmoja na Singida Black Stars, anatarajiwa kuwa mchezaji huru mara tu msimu utakapomalizika. Hali hiyo inafungua milango ya vilabu mbalimbali kumwania, ikiwemo Yanga ambao waliwahi kufaidika na huduma zake kwa misimu iliyopita.
Tangu kuondoka kwake Yanga, mashabiki na wachambuzi wamekuwa wakieleza kuwa nafasi yake kwenye kiungo cha ukabaji haijapata mbadala wa kudumu. Uimara wake, uzoefu na uwezo wa kuongoza safu ya kiungo vilikuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya timu hiyo.
Baada ya kuondoka kwake, Yanga ilijaribu kuongeza nguvu kwa kumsajili Moussa Balla Conte, lakini mchezaji huyo hakupata nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza. Hali hiyo ilisababisha aondoke kwa mkopo.
Baadaye, klabu hiyo ikamchukua kwa mkopo Mohamed Damaro “Ngosha” kutoka Singida Black Stars ili kuongeza nguvu eneo la kiungo cha ukabaji.
Kwa sasa, jukumu la kiungo mkabaji ndani ya Yanga linabebwa zaidi na Duke Abuya, huku Damaro pia akipata nafasi kwa vipindi. Hata hivyo, changamoto ya kadi na majeraha imekuwa ikipunguza uthabiti wa kikosi hicho eneo hilo.
Kuna uwezekano mkubwa kwamba Yanga watarejea sokoni kusaka kiungo mkabaji wa kiwango cha juu kuelekea msimu ujao. Jina la Aucho limeanza kuibuka tena kutokana na uzoefu wake na historia yake ndani ya klabu hiyo.
Aucho aliondoka Yanga baada ya mazungumzo ya mkataba kushindikana, ambapo alitaka mkataba wa miaka miwili, huku klabu ikitoa ofa ya mwaka mmoja pekee. Tofauti hiyo ilipelekea pande hizo mbili kuachana kwa makubaliano.



