Siku chache kuelekea Fainali za Kombe la Dunia 2026 nchini Marekani, Canada na Mexico, kocha wa timu ya taifa ya Uruguay, Marcelo Bielsa, amefanya maamuzi makubwa kwa kumwacha nje mshambuliaji mkongwe Luis Suárez katika kikosi cha mwisho cha wachezaji 26 kitakachoshiriki mashindano hayo.
Suárez, ambaye kwa sasa anacheza katika klabu ya Inter Miami, ameonyesha kiwango kizuri msimu huu wa Ligi Kuu ya Marekani (MLS) kwa kufunga mabao sita katika mechi 11. Hata hivyo, kiwango hicho hakikutosha kumshawishi Bielsa kumrudisha kwenye kikosi cha taifa kwa ajili ya mashindano hayo makubwa.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 39 alicheza mechi yake ya mwisho kwa Uruguay mwaka 2024. Katika historia ya soka la Uruguay, Suárez anabaki kuwa mfungaji bora wa muda wote akiwa amefunga mabao 69 katika mechi 143 za kimataifa. Ni Diego Godín pekee aliyewahi kuichezea Uruguay mechi nyingi zaidi, akiwa na mechi 161.
Mbali na Suárez, kiungo Nahitan Nández pia ameachwa nje ya kikosi hicho licha ya kuwa mmoja wa wachezaji waliotoa mchango mkubwa katika kampeni ya kufuzu Kombe la Dunia. Uamuzi huo umeibua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki na wachambuzi wa soka.
Kwa upande mwingine, Uruguay imepokea habari njema baada ya kurejea kwa kiungo wa Real Madrid, Federico Valverde, ambaye amepona majeraha na yuko tayari kuiongoza timu hiyo. Aidha, mshambuliaji Darwin Núñez anatarajiwa kuwa tegemeo kubwa katika safu ya ushambuliaji ya Uruguay.
Kipa mkongwe Fernando Muslera, mwenye mechi 134 za kimataifa, amerejea kwenye kikosi hicho na anatarajiwa kushiriki Kombe la Dunia lake la tano, huku beki wa Atlético Madrid, José María Giménez, akiwa karibu kufikisha mechi 100 akiwa na timu ya taifa.
Kikosi Kamili cha Uruguay (Wachezaji 26)
Makipa
Sergio Rochet
Fernando Muslera
Santiago Mele
Mabeki
Guillermo Varela
Ronald Araújo
José María Giménez
Santiago Bueno
Sebastián Cáceres
Mathías Olivera
Joaquín Piquerez
Matías Viña
Viungo
Manuel Ugarte
Emiliano Martínez
Rodrigo Bentancur
Federico Valverde
Agustín Canobbio
Juan Manuel Sanabria
Giorgian de Arrascaeta
Nicolás de la Cruz
Rodrigo Zalazar
Facundo Pellistri
Maximiliano Araújo
Brian Rodríguez
Washambuliaji
Rodrigo Aguirre
Federico Viñas
Darwin Núñez
Uruguay Wataanza Lini Kombe la Dunia?
Uruguay imepangwa Kundi H pamoja na Spain, Cape Verde na Saudi Arabia.
Mechi yao ya kwanza itachezwa dhidi ya Saudi Arabia tarehe 15 Juni 2026. Baadaye watacheza dhidi ya Cape Verde tarehe 21 Juni kabla ya kumalizia hatua ya makundi kwa mechi kubwa dhidi ya Hispania tarehe 26 Juni.
Licha ya kuachwa kwa Suárez, Uruguay bado ina kikosi chenye mchanganyiko wa uzoefu na nguvu ya vijana. Mashabiki wengi watakuwa na macho yao kwa Valverde, Núñez, Ronald Araújo na Manuel Ugarte huku timu hiyo ikisaka ubingwa wake wa kwanza wa Kombe la Dunia tangu mwaka 1950.



