Simba na Yanga kurejea mazoezini Jumatatu Juni 1

Joel JJ By Joel JJ β€’ 31st May 2026


Simba na Yanga kurejea mazoezini Jumatatu Juni 1

Vikosi vya vigogo wa soka Tanzania, Yanga SC na Simba SC, vinatarajiwa kurejea mazoezini Jumatatu Juni 1 baada ya mapumziko mafupi yaliotolewa kwa wachezaji kuelekea mwendelezo wa mechi za mwisho wa msimu wa Ligi Kuu na Kombe la CRDB.

Uongozi wa klabu ya Yanga SC uliwapa wachezaji mapumziko ya siku sita kufuatia ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Namungo FC, matokeo yaliyowapa morali kubwa katika mbio za kuhitimisha msimu kwa mafanikio.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa mabingwa hao wa nchi, Ali Kamwe, amesema kikosi hicho kitarejea kambini rasmi Jumatatu Juni 1 kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mechi zilizobaki za ligi pamoja na mashindano ya Kombe la CRDB.

Yanga SC imesalia na mechi tano muhimu za Ligi Kuu pamoja na mchezo wa nusu fainali ya Kombe la CRDB dhidi ya Azam FC.

Baada ya mapumziko ya kalenda ya FIFA, Yanga SC inatarajiwa kusafiri mkoani Kigoma kumenyana na Mashujaa FC Juni 13, kisha kuelekea Arusha kucheza dhidi ya Fountain Gate Juni 17.

Ratiba inaendelea kwa Wananchi kushuka uwanja wa CCM Kirumba Mwanza Juni 21 kuumana na Azam FC katika nusu fainali ya Kombe la CRDB, kabla ya kukutana tena na Azam FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Juni 24.

Mechi nyingine muhimu ni dhidi ya TRA United Juni 27 katika uwanja wa KMC Complex, na kisha kuhitimisha msimu dhidi ya JKT Tanzania uwanja wa Isamuhyo Juni 30.

Kwa upande wa Simba SC, kikosi hicho nacho kinatarajiwa kumaliza mapumziko ya siku saba Jumatatu na kurejea mazoezini kuanza maandalizi ya mechi za mwisho wa msimu.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ali, amesema wachezaji wote ambao hawana majukumu ya timu za taifa wanatarajiwa kuripoti kambini kwa ajili ya maandalizi hayo muhimu.

Simba SC imesalia na mechi tano za Ligi Kuu pamoja na mchezo wa nusu fainali ya Kombe la CRDB dhidi ya Coastal Union utakaopigwa Juni 20.

Kabla ya hapo, Simba itashuka dimba la KMC Complex Juni 14 kumenyana na Pamba Jiji, kisha kuelekea Mbeya kucheza dhidi ya Mbeya City Juni 17.

Ahmed Ali amesema klabu imejipanga kuhakikisha inamaliza msimu kwa nguvu na kupigania mataji yaliyosalia.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.