Uongozi wa klabu ya Azam FC unatajwa kuwa kwenye hatua za awali za mazungumzo na aliyekuwa kocha wa Young Africans SC, Pedro Gonçalves, ili aweze kuinoa timu hiyo kuelekea msimu ujao wa mashindano.
Taarifa zinaeleza kuwa Azam FC inamsaka mbadala wa Florent Ibenge, ambaye amefikia makubaliano na Shirikisho la Soka la Mali kwenda kuinoa timu ya taifa ya nchi hiyo.
Tangu alipoachana na Yanga, Gonçalves bado hajapata klabu au timu nyingine ya kuinoa. Hali hiyo imezidi kuongeza uwezekano wa kocha huyo kujiunga na Wanalambalamba hao wa Azam FC ikiwa mazungumzo yatafanikiwa.
Historia yake Yanga
Young Africans SC iliachana na Gonçalves mapema mwezi huu, mara baada ya mchezo dhidi ya KMC ambao Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0.
Licha ya kutopoteza mchezo wowote wa ligi katika kipindi chote alichokuwa akiinoa Yanga, uongozi wa klabu hiyo uliamua kumtoa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa mbinu zake hazikuendana na falsafa ya soka la timu hiyo.
Azam FC kuimarisha kikosi
Azam FC inaonekana kuingia sokoni kwa nguvu kubwa, ikilenga kupata kocha mwenye uzoefu wa kimataifa ili kuimarisha kikosi chake na kuongeza ushindani dhidi ya vigogo wa ligi kuu nchini Yanga na Simba.
Iwapo mazungumzo yatakamilika, Gonçalves atakuwa mmoja wa makocha waliowahi kuzinoa timu mbili kubwa zinazoshindana vikali kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, jambo linaloweza kuleta msisimko mpya kwenye ligi.



