Klabu ya Como, inayoongozwa na kocha wake Cesc Fàbregas, imeweka historia kubwa katika soka la Italia baada ya kufuzu kwa mara ya kwanza kabisa kwenye UEFA Champions League, kufuatia ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Cremonese katika mchezo wa mwisho wa Serie A.
Ushindi huo umeifanya Como kumaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi, na hivyo kujihakikishia tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2026/27.
Katika mchezo huo wa kihistoria, Como ilionyesha ubora mkubwa kupitia mabao ya Jesús Rodríguez, Tasos Douvikas na Lucas da Cunha, yaliyoihakikishia ushindi mnono dhidi ya Cremonese.
Cremonese walipata bao la kufutia machozi kupitia Federico Bonazzoli kwa penalti, lakini mambo yalizidi kuwa mabaya baada ya wachezaji wake watatu kuonyeshwa kadi nyekundu kufuatia vurugu zilizoibuka uwanjani.
Kocha Cesc Fàbregas, akizungumza baada ya mechi hiyo, alisema mafanikio hayo ni matokeo ya kazi kubwa ya kikosi cha vijana.
“Ni moja ya mafanikio makubwa zaidi kwangu, hasa kwa jinsi tulivyofanikisha hili na kikosi cha vijana wengi chini ya miaka 23,” alisema Fàbregas.
AC MILAN YAPOTEZA NAFASI YA CHAMPIONS LEAGUE
Matokeo ya mchezo huo yalienda sambamba na kipigo cha AC Milan cha mabao 2-1 dhidi ya Cagliari, kilichowagharimu nafasi ya Champions League.
Roma walifanikiwa kushinda na kumaliza katika nafasi ya tatu, huku Como ikiwapiku Milan katika mbio za nafasi ya nne ya mwisho.
JUVENTUS YAANGUKIA EUROPA LEAGUE
Katika upande mwingine, Juventus imeshindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kumaliza msimu nje ya Top 4, hivyo kuangukia UEFA Europa League msimu wa 2026/27.
Licha ya kuhitaji ushindi katika mchezo wao wa mwisho dhidi ya Torino, Juventus walilazimika kutoka sare ya mabao 2-2, ambapo Dusan Vlahovi aliwapatia uongozi wa mapema kabla ya Torino kusawazisha kupitia Cesare Casadei na Che Adams.
Matokeo ya Roma na Como yalithibitisha rasmi kuwa Juventus haitakuwa miongoni mwa timu zitakazoshiriki Champions League msimu ujao.



