Uchaguzi wa uongozi ndani ya klabu ya Real Madrid umesababisha kucheleweshwa kwa utambulisho wa kocha mpya, José Mourinho, ambaye alikuwa tayari kutangazwa rasmi kuchukua mikoba ya benchi la ufundi la miamba hiyo ya Hispania.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyombo vya habari vya Ulaya, Mourinho alitarajiwa kutangazwa rasmi leo kama kocha mpya wa Real Madrid, huku mipango yote ya sherehe za utambulisho ikiwa tayari imekamilika. Hata hivyo, mchakato huo umewekwa kiporo kutokana na hali ya kisiasa ndani ya klabu hiyo.
UCHAGUZI WABADILI MPANGO WA MADRID
Uongozi wa sasa chini ya Rais Florentino Pérez unakabiliwa na upinzani kutoka kwa mgombea mwingine, Enrique Riquelme, ambaye ameanzisha makao makuu ya kampeni yake karibu na Uwanja wa Santiago Bernabéu.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka Record, kama si mchakato wa uchaguzi, Mourinho angekuwa amethibitishwa rasmi kama kocha mpya wa Real Madrid.
Hata hivyo, kutokana na ushindani wa uchaguzi huo, tangazo la Mourinho limeahirishwa hadi baada ya matokeo rasmi yanayotarajiwa kutolewa tarehe 7 Juni.
MOURINHO KUSUBIRI MAAMUZI
Mourinho, ambaye aliondoka Madrid hapo awali akiwa na historia ya mafanikio na misuguano, aliondoka tena kwenda Lisbon jana akisubiri hatma yake mpya.
Kwa sasa, hatma yake ndani ya Santiago Bernabéu haijawa wazi, huku ikielezwa kuwa uteuzi wake unaweza kutegemea matokeo ya uchaguzi huo.
Endapo Florentino Pérez hatashinda uchaguzi huo, bado haijafahamika kama uongozi mpya utasonga mbele na mpango wa kumrejesha Mourinho au kuchagua kocha mwingine kabisa.



