Guardiola aagwa kwa heshima Manchester City

Joel JJ By Joel JJ • 25th May 2026


Guardiola aagwa kwa heshima Manchester City

Mashabiki wa Manchester City wameagana kwa hisia kubwa na kocha wao wa muda mrefu, Pep Guardiola, aliyemaliza rasmi safari yake ndani ya klabu hiyo baada ya zaidi ya miaka 10 ya mafanikio makubwa nchini England na barani Ulaya.

Katika mchezo wa mwisho wa msimu dhidi ya Aston Villa uliochezwa Etihad Stadium, hali ya uwanja ilitawaliwa zaidi na shughuli za kumuaga Guardiola kuliko matokeo ya mchezo wenyewe, ambapo City walipoteza kwa mabao 2-1.

Mashabiki wa City walionekana kubeba mabango, skafu na kuimba nyimbo maalum za kumpongeza kocha huyo Mhispania aliyebadilisha historia ya klabu hiyo tangu alipojiunga mwaka 2016.

MIAKA 10 YA MAFANIKIO MAKUBWA

Katika kipindi chake Manchester City, Guardiola ameandika historia kubwa kwa kushinda mataji 20 yakiwemo:

  • Mataji sita ya Premier League
  • UEFA Champions League
  • FA Cup
  • Kombe la Dunia la Vilabu
  • Carabao Cup kadhaa

Pia aliifanya City kuwa klabu ya kwanza katika historia ya England kushinda mataji manne ya Premier League mfululizo.

Manchester City pia imethibitisha kuwa itamuenzi Guardiola kwa kujenga sanamu lake pamoja na kutaja sehemu ya Etihad Stadium kwa jina lake kutokana na mchango wake mkubwa ndani ya klabu hiyo.

HISIA ZATAWALA ETIHAD

Baada ya filimbi ya mwisho, Guardiola alionekana akibubujikwa na machozi wakati akiwashukuru mashabiki wa City kwa sapoti waliompa kwa miaka yote aliyokaa Manchester.

Nyota wa City, Bernardo Silva, alimuelezea Guardiola kama:

“Baba wa soka” na “kocha bora wa muda wote.”

Katika hotuba yake ya mwisho mbele ya mashabiki, Guardiola alisema kuwa kipindi chake Manchester City kilikuwa cha kipekee na chenye kumbukumbu zisizofutika.

MWISHO WA ENZI YA DHAHABU CITY

Kuondoka kwa Guardiola kunahitimisha moja ya zama zilizofanikiwa zaidi katika historia ya Manchester City, ambapo aliibadilisha klabu hiyo kutoka timu ya ushindani wa kawaida hadi kuwa moja ya vilabu vikubwa zaidi duniani.

Mpaka sasa, Manchester City bado hawajamtangaza rasmi mrithi wa kocha huyo, huku mashabiki wengi wakiamini kuwa itakuwa vigumu kuziba pengo lake ndani ya klabu hiyo.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.