Kocha Mkuu wa Young Africans SC, Abdihamid Moalin, amemtetea nahodha wa kikosi hicho Bakari Nondo Mwamnyeto, akisisitiza kuwa hana mashaka na uwezo wake licha ya tukio la kujifunga lililotokea katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Dodoma Jiji FC uliochezwa mkoani Singida.
Katika mchezo huo, Mwamnyeto alijikuta akiujaza mpira kimakosa wavuni wakati akijaribu kuokoa hatari langoni, tukio lililosababisha mashabiki wengi kumkosoa kupitia mitandao ya kijamii.

Hata hivyo, Kocha Moalin amesema tukio hilo halipaswi kupunguza imani kwa beki huyo, akieleza kuwa makosa ni sehemu ya mchezo wa soka na maisha kwa ujumla.
“Kila mtu anamjua Bakari Mwamnyeto ni mchezaji mkubwa na mwenye heshima kubwa, siyo tu ndani ya Yanga bali pia kwenye soka la Tanzania kwa ujumla,” alisema Moalin.
“Siwezi kujadili uwezo wake kwa sababu ni jambo ambalo lipo wazi kwa kila mtu anayefuatilia mpira. Makosa ni sehemu ya maisha ya mwanadamu, siyo kwenye mpira pekee. Kama unaogopa kufanya makosa basi huwezi kuonyesha ubora wako wala kujiamini ukiwa uwanjani.”
“Wachezaji wakubwa duniani pia hufanya makosa, lakini kinachowatofautisha ni namna wanavyorudi na kupambana zaidi. Bakari ni kiongozi ndani na nje ya uwanja. Ana uzoefu mkubwa, anaipambania timu kila wakati na mchango wake kwa Yanga ni mkubwa sana,” aliongeza.
Kocha huyo ameendelea kusisitiza kuwa Mwamnyeto bado ni sehemu muhimu ya kikosi hicho na ataendelea kupewa sapoti na benchi la ufundi pamoja na viongozi wa klabu.
“Tuna imani kubwa naye na tunaendelea kumuunga mkono kwa sababu tunajua uwezo alionao na kile anachoweza kuifanya timu hii,” alihitimisha Moalin.
Licha ya presha kutoka kwa baadhi ya mashabiki baada ya tukio hilo, uongozi wa Yanga unaonekana kuendelea kusimama nyuma ya nahodha wao, ukiamini kuwa uzoefu wake bado ni muhimu katika msimu huu wa mashindano.



