Klabu ya Zamalek SC imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Misri kwa msimu wa 2025/26 baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ceramica Cleopatra FC katika mchezo wa mwisho wa msimu uliochezwa jijini Cairo.
Ushindi huo umeifanya Zamalek kufikisha pointi 56 na kutwaa taji lao la 15 katika historia ya ligi hiyo, baada ya ushindani mkali uliodumu hadi dakika za mwisho za msimu.
Katika msimamo wa mwisho, Pyramids FC walimaliza nafasi ya pili wakiwa na pointi 54 baada ya kushinda mchezo wao wa mwisho, huku Al Ahly wakimaliza nafasi ya tatu licha ya kuifunga Al Masry mabao 2-0.
Matokeo hayo yanamaanisha kuwa Zamalek na Pyramids FC wataiwakilisha Misri kwenye mashindano ya CAF Champions League msimu ujao, huku Al Ahly wakilazimika kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup).
Ni mara ya kwanza tangu mwaka 2003 kwa Al Ahly kukosa nafasi ya kushiriki CAF Champions League, jambo ambalo limezua mjadala mkubwa kutokana na historia kubwa ya klabu hiyo barani Afrika ambapo imewahi kutwaa taji hilo mara 12.
Msimu huu wa ligi kuu ya Misri ulikuwa na ushindani mkubwa kati ya timu hizo tatu hadi mzunguko wa mwisho, huku Zamalek wakifanikiwa kutumia vyema nafasi yao ya mwisho na kutwaa ubingwa mbele ya mahasimu wao wakubwa.



