Kiungo mkabaji wa Manchester United Casemiro, yuko mbioni kuhamia Ligi ya Marekani (MLS) msimu ujao baada ya taarifa za mazungumzo ya kujiunga na Inter Miami CF kuwa katika hatua za mwisho.
Ripoti kutoka kwa vyombo mbalimbali vya michezo Ulaya na Marekani zinaeleza kuwa Inter Miami imemuweka Casemiro kama chaguo lao kuu la kuimarisha eneo la kiungo baada ya kustaafu kwa Sergio Busquets mwishoni mwa msimu uliopita.
Nyota huyo wa Brazil mwenye umri wa miaka 34 anatarajiwa kuondoka Old Trafford mwishoni mwa msimu huu baada ya kuitumikia Manchester United kwa miaka minne tangu alipotua akitokea Real Madrid CF mwaka 2022.
Licha ya kuwa na kipindi kigumu katika baadhi ya mechi za hivi karibuni, Casemiro bado ameendelea kuonyesha uzoefu mkubwa na uongozi ndani ya kikosi cha United. Taarifa zinaeleza kuwa klabu hiyo imeamua kutompa mkataba mpya kutokana na umri wake pamoja na mshahara mkubwa anaolipwa kwa sasa.
Inter Miami, ambayo tayari ina mastaa kama Lionel Messi, Rodrigo De Paul na Germán Berterame, inaonekana kutaka kuongeza uzoefu zaidi katika kikosi hicho kinachowania kuendelea kutawala MLS. Klabu hiyo inayomilikiwa kwa sehemu na David Beckham inaamini Casemiro anaweza kuziba pengo lililoachwa na Busquets katikati ya uwanja.
Kulingana na sheria za mishahara za MLS, itamlazimu Casemiro kupunguza mshahara wake kwa kiasi kikubwa ili dili hilo likamilike.



