Yanga yaanza mipango ya kumrejesha Aziz Ki

Joel JJ By Joel JJ β€’ 20th May 2026


Yanga yaanza mipango ya kumrejesha Aziz Ki

Yanga imeingia katika hatua mpya ya mazungumzo ya kumrejesha aliyekuwa kiungo wake mshambuliaji, Stephan Aziz Ki, ambaye kwa sasa anaichezea Al Ittihad SC baada ya kuondoka Wydad AC, imefahamika.

Aziz Ki alisajiliwa na Wydad AC kutoka Yanga SC katika dirisha la usajili la msimu uliopita, lakini alidumu kwa kipindi kifupi cha takribani miezi sita kabla ya kuhamia Libya kujiunga na Al Ittihad SC katika usajili wa dirisha dogo la Januari 2026.

Taarifa zinaeleza kuwa Yanga SC imeanza mazungumzo ya siri ili kumshawishi kurejea Jangwani, huku vyanzo vikidai kuna maendeleo mazuri yanayoendelea nyuma ya pazia.

Kwa mujibu wa taarifa zisizo rasmi, Aziz Ki amekuwa akipitia changamoto za kiusalama nchini Libya, jambo linaloaminika kuchangia kuanza kufikiria kurejea Tanzania.

Aidha, sababu za kifamilia pia zimechangia msukumo huo. Nyota huyo kutoka Burkina Faso, mkewe Hamisa Mobeto yupo nchini Tanzania, hali inayomfanya atamani kuwa karibu na familia yake.

Aziz Ki na Hamisa Mobeto walifunga ndoa Februari 16, 2025 jijini Dar es Salaam. Tangu wakati huo, mchezaji huyo amekuwa akigawanya muda wake kati ya majukumu ya kikazi Libya na maisha ya kifamilia Tanzania, hali inayoripotiwa kumletea changamoto za kijamii na kisaikolojia kutokana na umbali.

Kabla ya kuondoka, Aziz Ki aliichezea Yanga SC kwa misimu mitatu ambapo aliweka rekodi ya kufunga zaidi ya mabao 50 katika mashindano mbalimbali. Pia alifanikiwa kutwaa tuzo za Mchezaji Bora (MVP) pamoja na kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Tanzania, akijijengea jina kama mmoja wa viungo washambuliaji bora kuwahi kucheza ligi ya Tanzania Bara.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.