Klabu ya Southampton FC imejikuta kwenye wakati mgumu baada ya kupewa adhabu kali na English Football League (EFL) kufuatia tuhuma za upelelezi dhidi ya wapinzani wao wa Championship play-offs.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya EFL, Southampton imeondolewa kwenye fainali ya Championship play-offs na pia imepewa adhabu ya kupokwa pointi nne zitakazotumika msimu wa 2026/27.
Kisa kilichoibua sakata hilo
Sakata hilo limepewa jina la “Spygate 2.0” baada ya madai kwamba baadhi ya wafanyakazi wa Southampton walinaswa wakirekodi mazoezi ya Middlesbrough FC kabla ya mchezo wa nusu fainali ya play-offs.
Ripoti zinaeleza kuwa uchunguzi wa EFL ulibaini Southampton walikiuka kanuni ya 127 ya ligi hiyo inayokataza timu kufuatilia au kurekodi mazoezi ya mpinzani ndani ya saa 72 kabla ya mchezo.
Mbali na Middlesbrough, uchunguzi pia ulidai kuwa Southampton walihusika kufuatilia mazoezi ya Oxford United na Ipswich Town katika baadhi ya mechi za msimu huu.
Adhabu yenye maumivu makubwa
Adhabu hiyo imekuwa pigo kubwa kwa Southampton kwa sababu ilikuwa imefuzu kucheza fainali ya kuwania kupanda Ligi Kuu England (Premier League), mchezo unaotajwa kuwa miongoni mwa mechi zenye thamani kubwa zaidi kifedha duniani.
Taarifa mbalimbali zinaonyesha timu inayopanda Premier League inaweza kupata zaidi ya pauni milioni 200 kupitia haki za matangazo, udhamini na mapato mengine.
Kutokana na adhabu hiyo, Middlesbrough sasa imerejeshwa kwenye fainali na itacheza dhidi ya Hull City katika pambano la kuwania kupanda daraja.
Southampton yapanga kukata rufaa
Uongozi wa Southampton tayari umetangaza kuwa utaendelea kushirikiana na EFL huku ukipanga kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.
Wachambuzi wa soka nchini England wanaamini sakata hili linaweza kuwa moja ya maamuzi makubwa zaidi kuwahi kutolewa katika historia ya Championship, hasa baada ya EFL kuamua kuchukua msimamo mkali tofauti na tukio la mwaka 2019 lililohusisha Leeds United ambapo timu hiyo iliishia kutozwa faini pekee.



