Kocha maarufu wa soka duniani, José Mourinho, ameripotiwa kufikia makubaliano ya kurejea katika klabu ya Real Madrid, kwa mujibu wa taarifa za mwandishi wa usajili, Fabrizio Romano.
Romano ameripoti kuwa Mourinho na uongozi wa Real Madrid wamekubaliana masharti yote ya mkataba mpya, huku hatua iliyosalia ikiwa ni kusaini nyaraka rasmi ndani ya mwezi huu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mkataba huo unatarajiwa kuwa wa awali wa miaka miwili, na masharti kati ya pande hizo mbili yakikubaliwa, jambo linaloashiria nia ya dhati ya pande zote katika kurejesha ushirikiano wao.
Inaelezwa kuwa Mourinho anatarajiwa kusafiri kuelekea Madrid mara baada ya mchezo wa Real Madrid dhidi ya Athletic Bilbao, ili kuanza rasmi maandalizi ya kuanza kazi katika awamu mpya ya kikosi hicho.
Mourinho si mgeni katika klabu hiyo, kwani aliwahi kuinoa Real Madrid na kuacha alama kubwa katika historia ya timu hiyo, hasa katika ushindani wa ndani ya La Liga na michuano ya Ulaya.
Kurejea kwake kunatajwa kuwa sehemu ya mpango wa klabu hiyo kuimarisha benchi la ufundi na kuongeza ushindani katika mafanikio ya ndani na ya kimataifa.
Mashabiki wa Real Madrid sasa wanasubiri kwa hamu kuona kama kocha huyo atarejea na mafanikio yaliyowahi kumfanya kuwa mmoja wa makocha wenye heshima kubwa duniani.



