Yanga SC wamefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la CRDB baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo wa robo fainali uliopigwa Uwanja wa Isamuhyo.
Mchezo huo ulianza kwa kasi, ambapo JKT Tanzania walionekana kuingia vizuri ndani ya dakika 15 za mwanzo wakisaka bao la mapema kwa presha kubwa dhidi ya mabingwa hao watetezi.
Hata hivyo, Yanga SC walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kujifunga kwa Hassan Wahabi katika dakika ya 33, baada ya kujaribu kuokoa krosi iliyopigwa na Chadrack Boka lakini akajikuta akiuweka mpira wavuni.
Dakika chache baadaye, Yanga walipata bao la pili dakika ya 40 kupitia kwa Mudathir Yahya, akimalizia kwa ustadi pasi iliyopangwa vizuri na Pacome Zouzoua ndani ya eneo la hatari.
Mabingwa hao watetezi walienda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-0, wakionekana kudhibiti mchezo na kujiamini zaidi.
Kipindi cha pili, Yanga waliendelea kutawala mchezo na kuunda nafasi kadhaa za kuongeza mabao, lakini umakini wa safu ya ulinzi ya JKT Tanzania uliwazuia kuongeza idadi ya mabao. Mpaka dakika 90 zinakamilika, matokeo yalibaki 2-0.
Kwa ushindi huo, Yanga SC sasa wameungana na Coastal Union ambao walitinga nusu fainali mapema baada ya kushinda kwa mikwaju ya penalti 4-2 dhidi ya Singida Black Stars baada ya sare tasa ya 0-0.
Katika hatua ya nusu fainali ya Kombe la CRDB, Yanga SC watakutana na mshindi wa pambano kati ya Mashujaa FC dhidi ya Azam FC, mechi ambayo inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Yanga SC wanaendelea kuonyesha ubora wao katika mashindano hayo, huku wakisalia na matumaini ya kutetea taji lao kwa mara ya tano mfululizo.



