Kocha Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, amesema anaamini kikosi chake kitakabiliana na mchezo mgumu dhidi ya TRA United katika hatua ya robo fainali ya Kombe la CRDB, huku akisisitiza kuwa maandalizi ya timu yake yamekamilika kwa kiwango kikubwa.
Simba SC itashuka dimbani kesho Jumapili, Mei 17, katika uwanja wa KMC Complex, kusaka tiketi ya kusonga mbele hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Barker alikiri ubora wa wapinzani wao TRA United, lakini akasisitiza kuwa kikosi chake kiko tayari kiakili na kimwili kwa changamoto hiyo.
“Tunakwenda kucheza dhidi ya timu nzuri na bora kwenye maeneo mengi, lakini sisi tumejiandaa kukabiliana na changamoto yoyote inayokuja mbele yetu,” alisema Barker.
“Morali ya wachezaji iko juu, tumefanya maandalizi mazuri kwa kuzingatia muda tuliopata. Tuko tayari kwenda kushinda mchezo huo,” aliongeza.
Simba SC na TRA United zinakutana kwa mara ya tatu msimu huu, baada ya timu hizo kukutana mara mbili kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara. Katika michezo hiyo, Simba ilishinda 3-0 katika mzunguko wa pili, huku mchezo wa kwanza ukimalizika kwa sare tasa ya 0-0 uliopigwa uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Mchezo wa kesho unatarajiwa kuwa mkali na wenye ushindani mkubwa kutokana na kuwa mchezo wa maamuzi kusaka tiketi ya nusu fainali ya Kombe la CRDB.



