Manchester City na Chelsea kulisaka taji la FA, fainali leo

Joel JJ By Joel JJ β€’ 16th May 2026


Manchester City na Chelsea kulisaka taji la FA, fainali leo

Macho ya mashabiki wa soka leo yataelekezwa katika dimba la Wembley ambapo vigogo wa England, Chelsea FC na Manchester City, watashuka dimbani kuwania ubingwa wa Kombe la FA msimu wa 2025/26.

Mchezo huo wa fainali unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa huku kila timu ikiwa na sababu tofauti ya kusaka ushindi mbele ya maelfu ya mashabiki watakaofurika uwanjani hapo.

Manchester City wanaonolewa na Pep Guardiola wanaingia kwenye mchezo huo wakisaka kuondoa kumbukumbu mbaya ya kupoteza fainali mbili zilizopita za mashindano hayo. City wamefanikiwa kufika fainali ya FA Cup kwa mara ya nne mfululizo, rekodi mpya katika historia ya klabu hiyo.

Licha ya kuwa miongoni mwa timu zilizoonesha kiwango bora msimu huu, Guardiola amesema ratiba ngumu ya mechi imeathiri maandalizi ya kikosi chake kuelekea pambano hilo muhimu.

Kwa upande wa Chelsea, mchezo huo unaonekana kuwa nafasi muhimu ya kuokoa msimu baada ya kushindwa kufanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali msimu huu.

Chelsea hawajatwaa taji la FA Cup tangu mwaka 2018 na pia wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa hawajapata ushindi dhidi ya Manchester City katika michezo 13 iliyopita.

Kocha wa muda wa Chelsea, Calum McFarlane, amesema kikosi chake kina morali ya kufanya vizuri licha ya wengi kuwapa nafasi ndogo ya kushinda mchezo huo.

Timu hiyo pia imepata habari njema baada ya baadhi ya nyota wake waliokuwa majeruhi kurejea kikosini kuelekea mchezo huo wa mwisho wa msimu.

Kwa mujibu wa takwimu za Chama cha Soka England (FA), hii ndiyo mara ya kwanza kwa Chelsea na Manchester City kukutana kwenye fainali ya FA Cup.

Chelsea wanatafuta ubingwa wao wa tisa wa mashindano hayo huku Manchester City wakisaka taji lao la nane.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.