Kocha Jose Mourinho anatajwa kuwa hatua za mwisho za kurejea kuinoa Real Madrid ambapo kulingana na Mwanahabari maarufu Fabrizio Romano, tayari amekubaliana na masharti yote ya mkataba wake mpya.
Fabrizio amebainisha kuwa mazungumzo kati ya Mourinho na rais wa Madrid, Florentino Pérez, yamekamilika kwa kiwango kikubwa huku kilichobaki kikiwa ni taratibu za mwisho kabla ya tangazo rasmi.
Mourinho ameweka masharti kadhaa muhimu kabla ya kurejea Santiago Bernabéu, ikiwemo uhuru mkubwa katika usajili wa wachezaji, maboresho ya kikosi pamoja na ushawishi mkubwa kwenye maamuzi ya kiufundi ndani ya klabu.
Kwa mujibu wa ripoti za hivi karibuni, uongozi wa Madrid umeonyesha utayari wa kukubaliana na matakwa hayo kutokana na presha ya kurejesha mafanikio ya haraka baada ya msimu wenye changamoto nyingi.
Vyanzo vya karibu na klabu vinaeleza kuwa Mourinho anaweza kutangazwa rasmi mara baada ya kumalizika kwa baadhi ya taratibu zinazomhusu na klabu yake ya sasa ya Benfica. Ripoti nyingine zinadai kuwa tayari kuna makubaliano ya muda wa mkataba pamoja na mipango ya usajili kwa ajili ya msimu ujao.
Mourinho aliwahi kuifundisha Real Madrid kati ya mwaka 2010 hadi 2013 ambapo aliisaidia kushinda mataji mbalimbali ikiwemo La Liga. Uongozi wa Madrid unaamini uzoefu wake mkubwa unaweza kurejesha nidhamu, ushindani na mafanikio ndani ya kikosi hicho.



