Vinara wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania, Simba Queens, wameendelea kuthibitisha ubora wao baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya watani zao Yanga Princess katika mchezo mkali uliopigwa kwenye uwanja wa Azam Complex.
Simba Queens walionyesha dhamira kubwa tangu dakika za mwanzo za mchezo huo, wakitawala sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza na kufanikiwa kupata mabao mawili kupitia mshambuliaji wao hatari, Jentrix Shikangwa. Mabao hayo yaliwapa Simba faida muhimu mapema.
Kocha wa Simba Queens, Mussa Mgosi, alionekana kuingia na mkakati wa kumaliza mchezo mapema. Kikosi chake kilicheza kwa kasi na presha kubwa kipindi cha kwanza kabla ya kubadili mfumo katika kipindi cha pili kwa kucheza kwa tahadhari zaidi na kutumia mashambulizi ya kushtukiza.
Kwa upande wa Yanga Princess, kipindi cha kwanza kilikuwa kigumu huku wakionekana kuchelewa kuingia mchezoni. Hata hivyo, walirejea kwa nguvu kipindi cha pili na kupata bao la kufutia machozi kupitia kwa Riticcia Nabossa dakika ya 58. Bao hilo lilitokana na mpira wa adhabu uliopigwa na Precious Christopher baada ya Jeaninne Mukandayisenga kufanyiwa madhambi karibu na eneo la hatari.
Tukio hilo lilizua mjadala mkubwa kwani baadhi ya mashabiki waliamini Yanga Princess walistahili kupata penalti badala ya faulo ya nje, huku pia wakitaka mwamuzi kutoa adhabu kali zaidi kwa mchezaji wa Simba Queens aliyehusika.
Licha ya Yanga Princess kuongeza mashambulizi kipindi cha pili, juhudi zao hazikuzaa matunda mbele ya safu imara ya ulinzi ya Simba Queens.
Matokeo hayo yanaifanya Simba Queens kuendelea kuongoza msimamo wa ligi kwa alama 46, hatua inayoweka timu hiyo kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa.
Kwa upande mwingine, Yanga Princess wamebaki nafasi ya pili wakiwa na alama 39, huku matumaini yao ya kuwania taji yakipungua baada ya kipigo hicho kutoka kwa watani zao.



