Simba yaunguruma Kigoma, yapunguza gap la pointi dhidi ya Yanga

Joel JJ By Joel JJ β€’ 14th May 2026


Simba yaunguruma Kigoma, yapunguza gap la pointi dhidi ya Yanga

Klabu ya Simba SC imeendelea kuonyesha makali yake kwenye mbio za ubingwa baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Mashujaa FC katika mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa dimba la Lake Tanganyika mkoani Kigoma.

Mnyama aliingia uwanjani akiwa na lengo moja tu, kuondoka na alama tatu muhimu, na haukusubiri muda mrefu kuonyesha ubora wake. Ilikuwa ni dakika ya tano pekee ambapo kiungo mahiri Clatous Chama alipoinyanyua Simba kwa bao la mapema kupitia kona ya moja kwa moja iliyomshinda mlinda lango wa Mashujaa FC.

Baada ya bao hilo, Simba iliendelea kutawala mchezo kwa kiwango kikubwa huku Mashujaa FC wakionekana kuzidiwa kasi na mbinu za wekundu hao wa Msimbazi. Mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa Simba yaliwapa wakati mgumu wenyeji hao ambao walijikuta wakilazimika kucheza zaidi eneo lao la kujilinda.

Mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika, Simba ilikuwa mbele kwa bao 1-0 huku mashabiki wake wakionekana kufurahia kiwango bora kilichoonyeshwa na timu yao.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ile ile kutoka kwa Simba, na tena alikuwa ni Chama aliyetikisa nyavu kwa mara ya pili kupitia shuti kali nje kidogo ya eneo la hatari. Bao hilo lilizidi kuthibitisha ubora wa kiungo huyo ambaye sasa ameweka rekodi ya kufunga mabao manne mfululizo kwenye ligi huku akifikisha mabao nane msimu huu.

Bao la tatu na la kufunga mchezo lilifungwa dakika za lala salama na Suleiman Mwalimu baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Neo Maema, akihitimisha usiku mzuri kwa Simba.

Ushindi huo unaifanya Simba kufikisha alama 52 kwenye msimamo wa ligi, ikiwa nyuma kwa tofauti ya alama mbili pekee dhidi ya watani zao Young Africans SC katika mbio kali za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kwa upande mwingine, Clatous Chama aliendelea kuwa gumzo baada ya kutwaa tena tuzo ya nyota wa mchezo, ikiwa ni mara yake ya nne mfululizo kufanya hivyo, jambo linaloonyesha kiwango chake bora ndani ya kikosi cha Simba kwa sasa.

Mapema mechi nyingine zilipigwa Mtibwa Sugar wakiibuka na ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya KMC katika mchezo ambao mabao 7 yalishuhudiwa huku Tanzania Prisons nayo ikiibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Fountain Gate na kufufua matumaini ya kwenye mapambano ya kujinusuru kushuka daraja.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.