Mikiki mikiki ya ligi kuu ya NBC inaendelea leo kuhitimisha raundi ya 23 ambapo mechi nne zinatarajiwa kupigwa katika viwanja mbalimbali.
Mechi mbili zinatarajiwa kupigwa mapema saa 8 Mtibwa Sugar ikiikaribisha KMC kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Morogogo huku Tanzania Prisons wakiumana na Fountain Gate dimba la Sokoine mkoani Mbeya.
Mchezo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka ni kati ya Mashujaa Fc dhidi ya Simba utakaopigwa saa 10:15 jioni katika uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.
Simba wakiwa ugenini wanasaka alama tatu ambazo zitawafanya wawasogelee watani zao Yanga kwenye mbio za ubingwa wa ligi kuu msimu huu.
Jana Yanga ilikubali kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa Dodoma Jiji na sasa ushindi kwa Simba utapunguza gap la pointi baina ya timu hizo kubaki mbili.
Hata hivyo Mashujaa Fc sio wanyonge wanapokuwa nyumbani kwani msimu huu hawajapoteza mchezo wowote dimba la Lake Tangayika.
Timu hiyo imecheza takribani mechi 7 bila ya kupoteza ikiwa chini ya kocha Jamhuri Kiwhelo 'Julio'.
Azam Fc na Pamba Jiji zitahitimisha mchezo wa nne utakaopigwa saa 12:30 jioni kwenye uwanja wa kMC Complex.




