Man City yaendelea kuibana Arsenal ubingwa EPL

Joel JJ By Joel JJ • 14th May 2026


Man City yaendelea kuibana Arsenal ubingwa EPL

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, Manchester City, wameendelea kuweka presha kubwa kwa vinara Arsenal baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Crystal Palace usiku wa Jumatano, Mei 13, 2026.

Katika mchezo huo uliopigwa dimba la Etihad, City walionyesha ubora mkubwa tangu kipindi cha kwanza huku Antoine Semenyo, Omar Marmoush na Savinho wakifunga mabao yaliyowapa ushindi muhimu sana kwenye mbio za ubingwa wa Premier League.

Baada ya ushindi huo, kikosi cha Pep Guardiola sasa kimefikisha alama 77 katika nafasi ya pili, nyuma ya Arsenal wenye alama 79 huku timu zote zikibakiwa na mechi mbili pekee kumaliza msimu.

Kiungo Phil Foden alikuwa nyota wa mchezo baada ya kutoa pasi mbili za mabao katika kipindi cha kwanza na kuiongoza City kucheza soka la kuvutia licha ya Guardiola kuwapa mapumziko baadhi ya nyota wake akiwemo Erling Haaland kuelekea fainali ya FA Cup mwishoni mwa wiki.

Guardiola amesema timu yake bado ipo hai kwenye mbio za ubingwa na itaendelea kupambana hadi mwisho wa msimu. Kocha huyo ana matumaini Arsenal wanaweza kupoteza pointi katika mechi zao mbili zilizobaki dhidi ya Burnley na Crystal Palace.

Kwa sasa, City wanahitaji kushinda mechi zao zote zilizobaki dhidi ya Bournemouth na Aston Villa huku wakisubiri makosa kutoka kwa Arsenal ili waweze kutwaa taji hilo kwa mara nyingine. 


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.