Goncalves, Okello watwaa tuzo za ligi kuu April

Joel JJ By Joel JJ β€’ 13th May 2026


Goncalves, Okello watwaa tuzo za ligi kuu April

Kiungo mshambuliaji wa Young Africans, ALLAN OKELLO, amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Aprili wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa mwaka 2025/26, huku PEDRO GONCALVES wa Young Africans, akichaguliwa Kocha Bora wa ligi hiyo kwa mwezi huo.

Okello alionesha kiwango kizuri chenye mwendelezo akiwashinda Pacome Zouzoua wa Yanga na Idd Selemani wa Azam FC, alioingia nao fainali katika mchakato wa tuzo za mwezi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Mchezaji huyo alitoa mchango mkubwa kwa timu yake katika michezo mitatu aliyocheza mwezi huo, akifunga bao moja na kuhusika na mengine sita kwa dakika 320 alizocheza.

Kwa upande wa Pedro aliyeingia fainali na Steve Barker wa Simba na Etiene Ndairagije wa TRA United, aliiongoza Young Africans kushinda michezo yote mitatu iliyocheza mwezi huo na kuendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa ligi, ikifunga mabao 12 na haikuruhusu bao. Young Africans ilizifunga Tanzania Prisons (3-0), Mbeya City (6-0) na Pamba Jiji (0-3).

Wakati huohuo Kamati ya Tuzo, imemchagua HASSAN MWATEREMA wa Kagera Sugar kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Aprili wa Ligi ya Championship ya NBC 2025/26, huku JUMA KASEJA pia wa Kagera Sugar akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo.

Mwaterema aliyeingia fainali na Japhet Mayungu wa TMA na Salum Mlemwa wa Gunners, alionesha kiwango chenye mwendelezo, ikiwa ni pamoja na kufunga mabao mawili kwa dakika 139 za michezo miwili aliyocheza.

Kwa upande wa Kaseja aliyeingia fainali na Zuberi Katwila wa Geita Gold na Mbwana Makata wa Polisi Tanzania, aliiongoza timu yake kushinda michezo yote miwili iliyocheza mwezi huo ikiendelea kubaki nafasi ya pili.

Pia Kamati ya Tuzo imeteua MAGOLI MATATU BORA ambayo yatapigiwa kura na mashabiki ili kupata goli bora la mwezi la mashabiki. Magoli hayo ni Pacome Zouzoua (Young Africans vs Mbeya City dakika ya 43), Idd Kipagwile (Dodoma vs Fountain Gate dakika ya 68) na Grayson Gwalala (Coastal v Dodoma Jiji dakika ya 14).


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.