Perez asisitiza haumwi, yuko fit kuiongoza Real Madrid

Joel JJ By Joel JJ ‱ 12th May 2026


Perez asisitiza haumwi, yuko fit kuiongoza Real Madrid

Rais wa Real Madrid Florentino Perez, ameweka wazi kuwa hana mpango wa kujiuzulu na badala yake atagombea tena nafasi ya urais wa klabu hiyo kubwa ya Hispania.

Akizungumza katika mkutano wa dharura na wanahabari uliofanyika leo Jumanne, Mei 12, 2026, Pérez alisema kuwa kuna kampeni maalum inayolenga kumchafua na kuivuruga Real Madrid, hasa baada ya klabu hiyo kupitia kipindi kigumu kisoka msimu huu.

“Kuna kampeni dhidi yangu, lakini sitajiuzulu. Bado nipo hapa na mimi ndiye rais wa Real Madrid,” alisema PĂ©rez mbele ya waandishi wa habari.

Perez pia alizungumzia uvumi uliosambaa kwenye mitandao ya kijamii ukidai kuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa saratani, akisema taarifa hizo ni za kutungwa na hazina ukweli wowote.

“Watu wengine wanasema nina saratani. Hizi taarifa zimetengenezwa tu. Afya yangu iko imara,” alisisitiza.

Mkutano huo wa ghafla uliibua taharuki kubwa miongoni mwa mashabiki wa Real Madrid, huku wengi wakidhani huenda Pérez angejiuzulu kutokana na presha inayotokana na matokeo mabaya ya timu hiyo msimu huu. Real Madrid inaelekea kumaliza msimu bila taji kubwa kwa mwaka wa pili mfululizo, hali iliyoongeza lawama kwa uongozi wake.

Katika hotuba yake, Pérez alieleza kuwa bado ana nguvu na nia ya kuendelea kuiongoza klabu hiyo, huku akitangaza kuwa uchaguzi mpya wa uongozi wa Real Madrid utafanyika mapema kuliko ilivyotarajiwa na yeye mwenyewe atawania tena nafasi hiyo.

Florentino Pérez mwenye umri wa miaka 79 amekuwa mmoja wa marais waliofanikiwa zaidi katika historia ya Real Madrid, akiiongoza klabu hiyo kushinda mataji mengi ikiwemo UEFA Champions League mara kadhaa katika vipindi vyake viwili vya uongozi. 


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.