Singida BS yaiongezea maumivu Namungo Fc

Joel JJ By Joel JJ β€’ 12th May 2026


Singida BS yaiongezea maumivu Namungo Fc

Singida Black Stars imepata ushindi muhimu wa bao 1-0 dhidi ya Namungo FC katika mchezo wa Ligi Kuu NBC uliopigwa kwenye Uwanja wa Airtel Mtipa mjini Singida, huku Mossi Ndumumwe akiwa shujaa kwa kufunga bao pekee la mchezo huo.

Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa ulishuhudia Singida BS wakitumia vizuri faida ya uwanja wa nyumbani na kupata bao muhimu lililowapa alama zote tatu muhimu katika harakati zao za kusalia kwenye nafasi za juu za msimamo wa ligi.

Mfungaji wa bao hilo pekee, Mossi Ndumumwe, aliibuka kuwa mhimili muhimu kwa Singida BS baada ya kufanikisha shambulizi lililoamua matokeo ya mchezo huo.

Kwa upande wa Namungo FC, kipigo hicho kinaendeleza hali mbaya ya matokeo kwa klabu hiyo ambayo sasa imefikisha michezo 13 mfululizo bila ushindi, ikiwa imesare mechi sita na kupoteza nyingine sita.

Takwimu zinaonyesha mara ya mwisho Namungo FC kushinda ilikuwa ni dhidi ya KMC FC waliposhinda bao 1-0 mwezi Januari 2026, bao likifungwa na Fabrice Ngoy.

Matokeo hayo yanaifanya Namungo FC kuendelea kujikuta kwenye wakati mgumu kwenye msimamo wa ligi, ikiwa nafasi ya 11 kwa pointi 24 baada ya kucheza mechi 23.

Kwa upande mwingine, Singida BS inaendelea kujikita kwenye mbio za kumaliza ndani ya nafasi nne za juu, ikiwa sasa inashika nafasi ya 4 ikiwa na pointi 38 baada ya kucheza mechi 23.

Katika mchezo mwingine kati ya TRA United dhidi ya JKT Tanzania uliopigwa uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha, timu hizo zimetoshana nguvu baada ya matokeo ya sare ya bao 1-1

Joseph Akandwanaho aliitanguliza TRA United dakika ya 20 kabla ya Salum Khamis kuisawazishia JKT Tanzania dakika ya 30.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.