Moalin apania alama tatu dhidi ya Dodoma Jiji

Joel JJ By Joel JJ • 12th May 2026


Moalin apania alama tatu dhidi ya Dodoma Jiji

Kocha Mkuu wa Yanga, Abdihamid Moalin, amesema maandalizi ya kikosi chake kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Dodoma Jiji FC yamekamilika kikamilifu, huku akisisitiza dhamira ya kupata pointi tatu muhimu.

Yanga inatarajiwa kushuka dimbani Jumatano katika Uwanja wa Airtel uliopo mkoani Singida, katika mchezo ambao una umuhimu mkubwa kwa vinara hao wa ligi wanaotafuta kujiimarisha zaidi kileleni mwa msimamo.

Moalin amesema kikosi chake kipo katika hali nzuri, isipokuwa beki Mohammed Hussein ‘Zimbwe Jr’ ambaye bado yuko chini ya uangalizi wa madaktari baada ya kurejea mazoezini akitokea kwenye majeraha.

Kocha huyo amekiri kuwa anatarajia mchezo mgumu dhidi ya Dodoma Jiji, lakini akasisitiza kuwa ana imani kubwa na ubora wa kikosi chake pamoja na maandalizi waliyofanya.

Ameongeza kuwa mazingira ya Uwanja wa Airtel yanaweza kuwapa faida kutokana na kufanana na Uwanja wa KMC Complex ambao Yanga wamekuwa wakitumia kama moja ya viwanja vyao vya nyumbani msimu huu.

Moalin amesema kila mchezo uliosalia msimu huu ni wa muhimu na hawana budi kucheza kwa tahadhari kubwa huku lengo likiwa moja tu—ushindi.

“Maandalizi yamekuwa mazuri. Mzunguko kati ya mechi ni mfupi sana, hivyo tulilazimika kuhakikisha wachezaji wanapata muda wa kupumzika na kuwa tayari kwa mchezo wa kesho. Tunatarajia mchezo mgumu lakini tumejiandaa,” alisema Moalin.

“Utakuwa mchezo wenye ushindani mkubwa dhidi ya Dodoma Jiji. Tunaamini mazingira ya uwanja yatatusaidia kwa kiasi fulani. Pamoja na ratiba ngumu, tunalenga pointi tatu.”

“Wachezaji wote wako salama isipokuwa Mohammed Hussein ambaye tunaendelea kumfuatilia. Pia Mudathir amerejea kikosini baada ya kumaliza adhabu yake ya kusimamishwa. Kila mchezo uliobaki ni muhimu sana kwetu,” aliongeza.

Yanga itaingia uwanjani ikiwa na lengo la kuendeleza ubabe wake kileleni mwa ligi, huku presha ya mbio za ubingwa ikiendelea kupamba moto.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.