Kocha Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, ameeleza kufurahishwa na kiwango cha kikosi chake baada ya ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Tanzania Prisons S.C. katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa katika Uwanja wa KMC Complex.
Huo ulikuwa mchezo wa kwanza kwa Simba kutumia dimba hilo jipya tangu kuhamisha mechi zao za nyumbani kutoka Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, hatua ambayo imeonekana kuleta mabadiliko chanya kwa timu hiyo.
Akizungumza baada ya mchezo, Barker alisema ubora wa uwanja wa KMC Complex umewasaidia wachezaji wake kutekeleza vyema mbinu za mchezo, huku akisisitiza kuwa kikosi chake kinaendelea kuelewa falsafa yake ya ufundishaji.
Alisema:
“Tulicheza kwenye uwanja mzuri ambao haukuwa na matuta mengi, hivyo hilo lilitusaidia sana. Tulianza mchezo vizuri, tukautawala kwa nguvu na intensiti ya juu.”
Kocha huyo aliongeza kuwa mabao waliyofunga yalikuwa matokeo ya uchezaji mzuri na wa kushirikiana, huku Simba wakiwazuia wapinzani wao kupata nafasi za hatari.
“Tulipofunga mabao yetu, yalikuwa ya kustahili kutokana na namna tulivyocheza. Tulidhibiti mchezo na kuwafanya wapinzani washindwe kupata nafasi,” alisema Barker.
Hata hivyo, alisema licha ya ushindi mkubwa, bado anaangalia ratiba ngumu iliyo mbele ya timu yake, akibainisha umuhimu wa usimamizi wa nguvu za wachezaji kutokana na michezo mingi mfululizo.
“Wakati mwingine unataka mabao mengi zaidi, lakini lazima usimamie nguvu. Tuna mechi nyingi ndani ya siku chache zijazo, hivyo tulihitaji kuwa makini,” aliongeza.
Baada ya ushindi huo, Simba inaelekea mkoani Kigoma kucheza dhidi ya Mashujaa FC katika Uwanja wa Lake Tanganyika, kabla ya kurejea Dar es Salaam kwa mchezo wa robo fainali ya Kombe la CRDB dhidi ya TRA United.



