Singida BS, JKT Tanzania, TRA United katika vita ya nne bora

Joel JJ By Joel JJ • 12th May 2026


Singida BS, JKT Tanzania, TRA United katika vita ya nne bora

Hesabu kali zinapigwa na makocha pamoja na wachezaji katika mechi za Ligi Kuu Bara zinazotarajiwa kuchezwa mikoa tofauti leo Jumanne, ambapo Singida Black Stars itakuwa nyumbani dhidi ya Namungo kwenye Uwanja wa Airtel, huku TRA United ikiikaribisha JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, huku kila timu ikiwania nafasi ya kupanda juu kwenye msimamo.

Kama Singida Black Stars iliyopo nafasi ya nne ikishinda dhidi ya Namungo, itaendelea kujiimarisha nafasi hiyo na itafikisha alama 38, lakini ikitokea ikapoteza na endapo JKT Tanzania iliyopo nafasi ya tano ikashinda dhidi ya TRA United, zitabadilishana nafasi.

Kwa sasa Singida Black Stars na JKT Tanzania zinalingana pointi zote zikiwa na 35, zinatofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, lakini TRA ina nafasi ya kuishusha JKT Tanzania nafasi ya tano kama itashinda mechi hiyo na kufikisha pointi 38.

Kwa upande wa Namungo iliyopo nafasi ya 11 katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 24, ikishinda mechi dhidi ya Singida BS itakuwa imefikisha alama 27 zitakazoishusha Fountain Gate yenye pointi 24 na Mashujaa iliyo na pointi 26, hivyo inaweza ikapanda hadi nafasi ya tisa.

Katika mechi nane walizokutana, Singida Black Stars imeshinda nne, Namungo imeshinda tatu, sare zikiwa mbili.

Kocha wa Singida BS, Muhibu Kanu, amesema: “Namungo ina wachezaji wazuri na wenye ushindani wa juu, inashambulia na kujilinda, lakini na sisi tumejipanga kuhakikisha tunavuna pointi tatu tukiwa nyumbani.”

Kwa upande wa nahodha wa Namungo, Jacob Masawe amesema: “Tupo nafasi mbaya kuliko Singida Black Stars kila mechi kwetu ni muhimu kushinda, tumejipanda na tupo tayari kupambana kwa kadri tutakavyoweza.”

TRA VS JKT TANZANIA

Achana na vita ya pointi tatu kufukuzia nafasi nne za juu, utamua wa mchezo wa TRA United dhidi ya JKT Tanzania ni kwa kukutana kwa makocha wa timu hizo, Ettiene Ndayiragije na Ahmad Ally katika sura tofauti.

Makocha hao wanakutana ikiwa ni takribani miaka saba tangu walipofanya kazi pamoja katika kikosi cha KMC mwaka 2019, kabla ya Ndayiragije aliyekuwa kocha mkuu kutimkia Azam na kumuacha msaidizi wake huyo akiendelea na majukumu.

Ndayiragije raia wa Burundi ndiye alimtambulisha rasmi Ahmad katika Ligi Kuu mwaka 2017 alipoamua kumvuta katika kikosi cha Mbao FC akitokea kituo cha michezo cha Marsh Athletes kilichopo mitaa ya Mirongo jijini Mwanza wakati akiinoa Marsh Queens.

Baada ya kufanya kazi kwa mafanikio katika kikosi cha Mbao, Ndayiragije alipata dili la kutua KMC ambapo aliamua kuondoka na benchi lake, akiwamo Ahmad na kocha wa viungo Faraji Muya.

Kocha huyo baada ya kufanya kazi Azam kwa muda mfupi, aliitwa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kabla ya kuondoka tena nchini kwao kabla ya kujiunga na Police FC ya nchini Kenya na kisha TRA United kumrejesha Tanzania.

Hata hivyo, uhondo wa mchezo huo ambao utapigwa kesho Jumanne kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, unavuta hisia kali kwa makocha na timu hizo kuwania pointi tatu kujiweka nafasi nne za juu.

Msimu huu TRA United (zamani Tabora United) na JKT Tanzania zimeonekana kuwa na moto mkali kwa ushindani unaooneshwa na wababe hao na kuweka vita ya kusaka nafasi ya kuwakilisha nchi kimataifa mwakani.

Timu hizo zimekuwa bora kwenye mashindano yao msimu huu kwani mbali na kukimbizana kwenye nafasi nne za juu, wababe hao wamefuzu nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB wakiungana na Yanga, Simba, Azam na Mashujaa.

Hadi sasa JKT Tanzania wapo nafasi ya tano kwa pointi 35 wakiwa na wastani wa bao moja, huku wapinzani TRA United wakiwa nafasi ya sita kwa pointi 33 na wastani wa mzuri wa mabao saba ya kufunga.

Akielezea mchezo huo, Ahmad Ally amesema vijana wake wako tayari akieleza kuwa wamejiandaa kiakili, kisaikolojia na kiufundi dhidi ya TRA United akikiri ugumu wake. “Tunaona vita ya pointi kwenye msimamo lakini tuko tayari kwa mchezo huo japokuwa tunafahamu ugumu ila tutaenda kwa mipango dhidi ya wapinzani hao, wachezaji wangu wako imara,” amesema kocha huyo.

Kwa upande wake Ndayiragije amesema malengo yake ni kuitambulisha timu hiyo kwenye mashindano ya kimataifa, akibainisha kuwa kila mchezo kwao ni vita ya pointi tatu ili kufikia ndoto zao.

Mwanaspoti


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.