Baada ya miaka 16 tangu walipokutana kwenye mchezo wa ufunguzi wa Kombe la Dunia 2010 nchini Afrika Kusini, sasa Mexico na South Africa wanatarajiwa kuandika ukurasa mwingine wa historia katika mchezo wa kwanza wa Kombe la Dunia 2026.
Mchezo huo mkubwa utapigwa Juni 11, 2026 ndani ya dimba maarufu la Estadio Azteca jijini Mexico City, ukiwa ndio utakaofungua rasmi mashindano hayo makubwa yatakayofanyika kwa pamoja nchini Mexico, Marekani na Canada.
Mashabiki wengi wa soka duniani tayari wameanza kuuita mchezo huo kama “marudio ya historia”, kutokana na kumbukumbu ya sare ya mabao 1-1 iliyotokea mwaka 2010 wakati Afrika Kusini walipokuwa wenyeji wa mashindano hayo.
Katika mchezo huo wa kihistoria, Siphiwe Tshabalala aliifungia Afrika Kusini bao lililobaki kwenye kumbukumbu za Kombe la Dunia kabla ya Rafael Márquez kuisawazishia Mexico.
Safari hii mazingira ni tofauti kabisa.
Mexico wanaingia mashindanoni kama wenyeji huku wakibeba matumaini makubwa ya kufanya vizuri mbele ya mashabiki wao. Kocha Javier Aguirre tayari ameanza maandalizi ya awali ya kikosi chake kwa kuweka kambi maalum na michezo ya kirafiki kuelekea mashindano hayo.
Kwa upande wa Afrika Kusini, maarufu kama Bafana Bafana, mchezo huo unaonekana kama nafasi ya kuonyesha dunia kuwa soka la Afrika bado lina ushindani mkubwa kwenye majukwaa makubwa.
Kundi A la mashindano hayo pia linazikutanisha Mexico na Afrika Kusini pamoja na South Korea na Czech Republic , jambo linalofanya mchezo wa ufunguzi kuwa muhimu sana katika mbio za kusaka tiketi ya hatua inayofuata.
Mbali na mchezo wenyewe, FIFA pia imeandaa shamrashamra kubwa za ufunguzi zitakazohusisha burudani kutoka kwa wasanii maarufu duniani. Ripoti zinaeleza kuwa mastaa kama Tyla, J Balvin na kundi la Maná watakuwa sehemu ya hafla hiyo kubwa kabla ya mpira kuanza.
Dimba la Estadio Azteca litakuwa linaandika historia nyingine muhimu kwani litakuwa uwanja wa kwanza duniani kuwahi kuandaa michezo ya Kombe la Dunia katika matoleo matatu tofauti 1970, 1986 na sasa 2026.
Kwa Mexico, huu ni mchezo wa kulipa kisasi cha kushindwa kupata ushindi kwenye michezo mingi ya ufunguzi wa Kombe la Dunia licha ya kuwa moja ya mataifa yaliyoshiriki mechi nyingi za ufunguzi katika historia ya mashindano hayo.
Lakini kwa Afrika Kusini, hii ni nafasi ya kurejesha kumbukumbu nzuri za mwaka 2010 na kuanza mashindano kwa mshangao mkubwa mbele ya mataifa yenye nguvu duniani.
Swali kubwa linalobaki sasa ni hili:
Je, Mexico watautumia uwanja wa nyumbani kuanza kwa ushindi, au Afrika Kusini wataandika historia nyingine kubwa kwenye mchezo wa ufunguzi wa Kombe la Dunia 2026?



