Kiungo mshambuliaji wa Simba SC, Clatous Chama maarufu kama ‘Mwamba wa Lusaka’, ameendelea kudhihirisha kiwango chake bora ndani ya kikosi hicho baada ya kutwaa tuzo ya nyota wa mchezo katika mechi tatu mfululizo.
Nyota huyo raia wa Zambia ameonyesha kuwa ni mhimili mkubwa wa mafanikio ya Simba katika michezo ya hivi karibuni, akihusika moja kwa moja kwenye mabao muhimu yaliyoiwezesha timu yake kuendelea kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
Jana, akiiongoza Simba kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Tanzania Prisons, Chama alifunga bao moja na kutoa pasi ya usaidizi wa bao jingine, jambo lililomfanya aondoke tena na tuzo ya Man of the Match.
Mwamba huyo wa Lusaka sasa amefunga katika mechi tatu mfululizo huku kila mchezo akiondoka na tuzo ya mchezaji bora wa mechi.
Mnamo Mei 03, kwenye dabi kali dhidi ya Yanga iliyomalizika kwa sare ya mabao 2-2, Chama aling’ara kwa kufunga bao na kutoa pasi ya bao kabla ya kutwaa tuzo ya nyota wa mchezo baada ya dakika 90 kukamilika.
Baadaye Mei 06, katika mchezo dhidi ya JKT Tanzania uliochezwa Dimba la Meja Jenerali Isamuhyo, kiungo huyo alifunga bao pekee lililoipa Simba ushindi wa bao 1-0 na pointi tatu muhimu, huku akichukua tena tuzo ya mchezaji bora wa mechi.
Dhidi ya Prisons jana, Chama alifikisha mabao sita msimu huu sambamba na asisti nne tangu kurejea kwake Msimbazi katika dirisha dogo la usajili.
Tangu arejee ndani ya kikosi cha Simba, Chama tayari ametwaa jumla ya tuzo tano za nyota wa mchezo, ishara ya kiwango chake kikubwa na mchango wake ndani ya timu hiyo.



