Arsenal FC wameendelea kuweka hai matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England baada ya kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya West Ham United katika mchezo wenye drama kubwa ya VAR uliopigwa London Stadium.
Mchezo huo ulikuwa mgumu kwa pande zote mbili huku Arsenal wakihitaji ushindi ili kuendelea kuishinikiza mbio za ubingwa. Bao pekee la ushindi lilifungwa na Leandro Trossard dakika ya 83 baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Martin Odegaard.
Dakika za mwisho za mchezo ziligeuka kuwa gumzo baada ya West Ham kuamini kuwa wamepata bao la kusawazisha kupitia Callum Wilson katika muda wa nyongeza. Hata hivyo, baada ya ukaguzi mrefu wa VAR, mwamuzi Chris Kavanagh aliamua kulikataa bao hilo kutokana na faulo dhidi ya kipa wa Arsenal David Raya kwenye harakati za kuwania mpira wa kona.
Uamuzi huo umeibua mjadala mkubwa England, huku baadhi ya wachambuzi wakidai ilikuwa moja ya maamuzi makubwa zaidi ya VAR katika mbio za ubingwa wa Premier League msimu huu.
Kwa ushindi huo, Arsenal wameendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa ligi na kuongeza matumaini ya kutwaa ubingwa wao wa kwanza wa Premier League tangu mwaka 2004.
Arsenal wamefikisha alama 79 wakisalia na mechi mbili huku Man City wakiwa na alama 74 na mechi tatu mkononi.



