Simba yaifumua Prisons 4-0, KMC mambo magumu

Joel JJ By Joel JJ • 10th May 2026


Simba yaifumua Prisons 4-0, KMC mambo magumu

Mikiki mikiki ya Ligi Kuu NBC imeendelea leo kwa michezo mitatu kupigwa katika viwanja tofauti huku vigogo wa soka wakioneshana ubabe.

Mapema kabisa, KMC FC waliendelea kubaki kwenye wakati mgumu baada ya kupokea kichapo cha mabao 3-2 kutoka kwa Fountain Gate FC katika mchezo uliochezwa Uwanja wa KMC Complex.

Kipigo hicho kinaendelea kuwaweka KMC katika hatari kubwa ya kushuka daraja huku wakisalia mkiani mwa msimamo wa ligi. Licha ya kuonyesha ushindani katika baadhi ya dakika za mchezo huo, Fountain Gate walikuwa makini zaidi kutumia nafasi walizozipata.

Katika mchezo mwingine, Pamba Jiji FC walilazimishwa suluhu ya bila kufungana dhidi ya Dodoma Jiji FC katika mechi iliyokuwa na ushindani mkubwa lakini ikakosa ubora wa kumalizia nafasi langoni.

Wakati huo huo, Simba SC wametoa tamko zito baada ya kuitandika Tanzania Prisons mabao 4-0 katika mchezo uliopigwa KMC Complex.

Tangu dakika za mwanzo, Simba walionyesha dhamira ya kutaka ushindi mkubwa huku wakitawala mchezo kwa kiwango kikubwa. Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa Wekundu wa Msimbazi kuwa mbele kwa mabao 3-0 yaliyofungwa na Morice Abraham, Clatous Chama na Suleiman Mwalimu.

Kipindi cha pili Simba waliendelea kushambulia kwa kasi, huku Ismail Toure akiandika bao la nne lililohitimisha karamu ya mabao kwa Simba.

Ushindi huo ungeweza kuwa mkubwa zaidi kama Simba wangekuwa makini kutumia nafasi nyingi walizozitengeneza mbele ya lango la Prisons.

Kwa ushindi huo, Simba wamefikisha alama 49 na kuendelea kujiimarisha katika nafasi ya pili ya msimamo wa ligi, huku tofauti ya pointi dhidi ya vinara Yanga ikibaki kuwa alama tano.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.