USM Alger yapata ushindi mwembamba dhidi ya Zamalek fainali ya kwanza CAFCC

Joel JJ By Joel JJ • 10th May 2026


USM Alger yapata ushindi mwembamba dhidi ya Zamalek fainali ya kwanza CAFCC

Klabu ya USM Alger imepata ushindi muhimu wa mabao 1-0 dhidi ya Zamalek SC katika mchezo wa kwanza wa fainali ya CAF Confederation Cup uliochezwa Jumamosi usiku, Mei 09, 2026, kwenye dimba la Stade du 5 Juillet.

Mchezo huo ulikuwa na ushindani mkubwa kutoka kwa timu zote mbili, huku mashabiki waliokuwa wamejaa uwanjani wakishuhudia pambano kali la kimbinu kati ya vigogo hao wa Afrika Kaskazini.

Bao pekee la mchezo lilifungwa na mshambuliaji Ahmed Khaldi dakika ya 90+8 kupitia mkwaju wa penalti uliotokana na maamuzi ya VAR yaliyowagharimu Zamalek mwishoni mwa mchezo.

Dakika za mwisho za mchezo zilikuwa za kusisimua sana baada ya Zamalek kuamini wamepata bao la ushindi kabla ya mwamuzi kusitisha mchezo na kwenda kuangalia VAR.

Baada ya mapitio hayo, penalti ilitolewa kwa USM Alger na Ahmed Khaldi hakufanya makosa, akitikisa nyavu na kuwapa Waarabu hao wa Algeria ushindi mwembamba lakini muhimu kuelekea mchezo wa marudiano.

Ushindi huo unaifanya USM Alger kuwa katika nafasi nzuri kabla ya safari ya kwenda Cairo kwa mchezo wa pili utakaopigwa Mei 16, 2026 kwenye Cairo International Stadium. Hata hivyo, Zamalek bado wana nafasi ya kurejea kwani watakuwa nyumbani wakihitaji ushindi wa zaidi ya bao moja ili kutwaa ubingwa huo wa CAF Confederation Cup.

Kocha wa USM Alger, Lamine N’Diaye, alisisitiza umuhimu wa kutumia faida ya nyumbani kabla ya mchezo huo, huku upande wa Zamalek chini ya Motamed Gamal ukiamini uzoefu wao wa michuano ya Afrika unaweza kuwasaidia kufanya vizuri ugenini.

Kwa upande wa historia, USM Alger wanatafuta taji lao la pili la CAF Confederation Cup baada ya kutwaa ubingwa mwaka 2023 walipoifunga Young Africans SC, wakati Zamalek wakisaka kuongeza mataji yao baada ya kutwaa ubingwa huo mwaka 2019 na 2024.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.