Simba yafuata mshambuliaji DR Congo

Joel JJ By Joel JJ • 8th May 2026


Simba yafuata mshambuliaji DR Congo

Klabu ya Simba SC inaendelea kujiimarisha kuelekea msimu ujao, ambapo sasa imeelezwa kuwa inamfuatilia mshambuliaji wa klabu ya FC Saint-Éloi Lupopo, Henoc Molia, anayesifika kwa kiwango bora katika Ligi Kuu ya DR Congo.

Taarifa zinaeleza kuwa Simba SC imeonyesha nia ya kumsajili Molia, ambaye kwa sasa anaichezea Lupopo na amekuwa mmoja wa wachezaji waliovutia zaidi msimu huu.

Mshambuliaji huyo ameonyesha kiwango cha juu akiwa amefunga mabao 13 na kutoa asisti 9, takwimu zinazomfanya kuwa miongoni mwa wachezaji hatari zaidi kwenye ligi hiyo.

Molia ambaye ana uwezo wa kucheza kama mshambuliaji wa kati au winga wa kushoto na kulia, alijiunga na Lupopo msimu uliopita akitokea AC Rangers, na sasa inaelezwa anafikiria changamoto mpya nje ya DR Congo.

Simba kufanya maboresho safu ya ushambuliaji

Simba SC inatarajiwa kufanya mabadiliko makubwa katika safu yake ya ushambuliaji kutokana na kutokuwepo kwa uthabiti wa mabao katika michezo ya karibuni.

Kocha mkuu wa Simba, Steve Barker, amekuwa akilazimika kubadilisha mfumo wa timu mara kadhaa akicheza bila mshambuliaji wa asili katika baadhi ya mechi.

Kwa sasa, ni Suleiman Mwalimu pekee anayetegemewa sana katika nafasi hiyo, ingawa naye yupo kwa mkopo na mustakabali wake bado haujafahamika wazi.

Inaelezwa kuwa Mwalimu anaweza kurejea katika klabu yake ya Wydad AC endapo makubaliano mapya hayatafikiwa kati ya pande zote mbili.

Hatma ya Jonathan Sowah ndani ya Simba

Wakati huo huo, mshambuliaji kutoka Ghana, Jonathan Sowah, naye anaonekana kuwa katika wakati mgumu baada ya kuingia kwenye mtafaruko na viongozi wa Simba.

Inaelezwa kuwa licha ya kuagizwa kufanya mazoezi na kikosi cha vijana, Sowah amegoma kufanya hivyo hali inayozidi kuashiria uwezekano wa kuondoka klabuni hapo.

Uongozi wa Simba SC unaonekana kutafuta suluhisho la muda mrefu katika safu ya ushambuliaji ili kuhakikisha timu inakuwa na uwiano mzuri wa mabao msimu ujao.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.