Rooney ampigia chapuo Carrick akabidhiwe mikoba Man United

Joel JJ By Joel JJ • 8th May 2026


Rooney ampigia chapuo Carrick akabidhiwe mikoba Man United

Nguli wa zamani wa Manchester United, Wayne Rooney, ameendelea kusisitiza kuwa Michael Carrick anastahili kupewa nafasi ya kudumu ya kuinoa klabu hiyo kufuatia matokeo mazuri aliyoyapata tangu alipopewa jukumu la kuinoa timu hiyo kwa muda.

Rooney amesema Carrick ameonyesha uwezo mkubwa wa kiuongozi kwa kuirejesha Manchester United kwenye ushindani ndani ya muda mfupi, huku akieleza kuwa mafanikio yake hayapewi uzito unaostahili kwa sababu ni kocha mchanga na raia wa Uingereza.

“Kama Manchester United wangemleta Luis Enrique au Thomas Tuchel na wakashinda michezo 10 kati ya 14 mfululizo, kila mtu angesema jambo la ajabu na kumsifia kwa kila aina ya sifa. Michael Carrick kafanya hivyo na hakuna anayemsifia kwa sababu ni kocha mchanga na ni Muingereza anapuuzwa,” alisema Rooney.

Rooney ambaye aliwahi kucheza pamoja na Carrick kwa mafanikio makubwa ndani ya Manchester United, amesema kocha huyo anaifahamu vyema DNA ya klabu hiyo na ana uwezo wa kuiongoza kwa muda mrefu.

“Michael Carrick ni mtu mwelevu sana, ni kocha mzuri sana na nadhani anaweza kuiongoza timu kwa muda mrefu tu. Tangu timu iwe chini yake Manchester United imepata utulivu na mashabiki sasa wanafurahia matokeo.”

Tangu apewe jukumu la kuiongoza timu hiyo mapema mwaka huu baada ya kuondoka kwa kocha wa zamani, Carrick ameiongoza United kushinda michezo 10 kati ya 14 kwenye ligi, rekodi iliyowafanya wengi kuanza kumtaja kama chaguo sahihi la kudumu Old Trafford.

Chini ya Carrick, Manchester United imefanikiwa kupata ushindi dhidi ya vigogo kama Manchester City, Liverpool FC, Chelsea FC na Arsenal FC, huku ikipewa nafasi kubwa ya kumaliza ndani ya nne bora na kurejea kwenye michuano ya UEFA Champions League msimu ujao.

Katika mahojiano tofauti, Carrick mwenyewe amesisitiza kuwa bado ameweka akili yake kwenye kuisaidia timu kumaliza msimu vizuri licha ya mjadala mkubwa unaoendelea kuhusu hatma yake ndani ya klabu hiyo.

Mashabiki wengi wa Manchester United wameonekana kumuunga mkono Carrick kutokana na mabadiliko ya haraka ya kiwango cha timu, huku baadhi wakiamini kuwa kurejesha utambulisho wa klabu hiyo kunahitaji mtu anayeifahamu vizuri historia na tamaduni za United kama Carrick.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.