Moalin apania ushindi wa kwanza dhidi ya Coastal Union

Joel JJ By Joel JJ • 8th May 2026


Moalin apania ushindi wa kwanza dhidi ya Coastal Union

Kocha Mkuu mpya wa Yanga, Abdilhamid Moalin, amesema yupo tayari kuanza kazi rasmi kwa ushindi pale timu yake itakaposhuka dimbani kesho kuivaa Coastal Union katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa kwenye KMC Complex.

Moalin ambaye amekabidhiwa mikoba iliyoachwa na Pedro Goncalves, amesema maandalizi ya mchezo huo yamekamilika kwa kiwango kizuri huku akionesha kujiamini kuwa kikosi chake kitaonyesha kiwango bora mbele ya mashabiki wa Yanga.

Kocha huyo wa zamani wa Azam FC na KMC FC amesema wachezaji wote wako tayari kwa pambano hilo muhimu na wanaelewa matarajio makubwa ya mashabiki wa mabingwa hao watetezi wa ligi kuu.

“Maandalizi ya mchezo wa Coastal Union yamefanyika salama. Kila mchezaji yupo imara kukabiliana na mchezo huo. Nina matumaini na vijana wetu kuwa watatupatia kila kilicho bora. Ukweli ni kwamba vijana wanajua mashabiki wanataka nini. Kila mchezaji anapaswa kuweka akili yake kwenye mchezo wa kesho,” alisema Moalin.

Mbali na kuahidi ushindi, Moalin amesema mashabiki wa Yanga wanapaswa kutarajia kuona timu yao ikicheza soka la kushambulia na kumiliki mchezo kwa dakika zote 90.

“Kitu ninachoweza kuwaahidi mashabiki wa Yanga ni mchezo mzuri. Sisi kama Yanga tuna namna yetu ya mchezo. Msingi wa Yanga ni kumiliki mchezo. Tunawaheshimu Coastal Union lakini hatuwezi kuacha utamaduni wetu. Tunataka kumiliki dimba, sio kwa dakika chache bali kwa dakika zote 90,” aliongeza.

Aidha, kocha huyo amesisitiza kuwa licha ya kujiamini, hawaichukulii poa Coastal Union kutokana na ubora wa kikosi hicho, huku akieleza kuwa bado ana muda mchache wa kufanya mabadiliko makubwa ndani ya timu tangu achukue majukumu hayo mapya.

“Niwe mkweli, Coastal Union ni timu nzuri. Tunawaheshimu sana kama ambavyo tunaheshimu wapinzani wengine. Vijana wetu wanaelewa kabisa kuwa huu sio mchezo rahisi. Tuna muda mchache sana wa kubadilisha vitu kwenye timu yetu. Tutatumia muda mchache uliopo kurekebisha machache yanayorekebishika,” alisema.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.