Nyota wa Real Madrid CF Kylian Mbappé, ameripotiwa kuwa tayari kurejea uwanjani kuelekea mchezo mkubwa wa El Clásico dhidi ya FC Barcelonautakaopigwa Jumapili, May 10 baada ya kufaulu vipimo vya afya vilivyofanywa na madaktari wa klabu hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka COPE na vyombo vingine vya michezo vya Hispania, Mbappé ameonyesha maendeleo makubwa katika kupona majeraha ya misuli ya mguu wa kushoto yaliyokuwa yakimuweka nje ya baadhi ya michezo ya hivi karibuni ya La Liga.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa alishiriki sehemu ya mazoezi ya pamoja na kikosi cha Real Madrid leo, jambo lililoongeza matumaini ya kuwepo kwake katika kikosi kitakachoivaa Barcelona kwenye mchezo huo mkubwa.
Mashuhuda kutoka mazoezini wamedai Mbappé alionekana akiwa na furaha na hali nzuri muda alipokuwa akiondoka kambini baada ya mazoezi, ishara inayotafsiriwa kuwa amejiandaa kurejea vitani katika kipindi muhimu cha msimu.
Awali kulikuwa na hofu kubwa kuhusu uwepo wake baada ya kupata majeraha kwenye mchezo dhidi ya Real Betis, hali iliyomfanya kukosa mchezo mmoja wa ligi huku akiendelea na programu maalum ya matibabu na mazoezi binafsi.
Hata hivyo, taarifa za sasa zinaonyesha benchi la ufundi la Real Madrid lina matumaini makubwa ya kumtumia nyota huyo dhidi ya Barcelona, mchezo unaotajwa kuwa muhimu kwa heshima ya Real Madrid ambayo haiko tayari Barcelona kutwaa ubingwa mbele yao.



