Singida BS yaanza na kinda mfungaji bora DR Congo

Joel JJ By Joel JJ • 7th May 2026


Singida BS yaanza na kinda mfungaji bora DR Congo

Klabu ya Singida Black Stars imeanza harakati za kuimarisha safu yake ya ushambuliaji kuelekea msimu ujao baada ya kuripotiwa kutuma ofa rasmi kwa klabu ya AS Dauphin Noir ya DR Congo kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji chipukizi, Candidat Mapendo.

Mapendo mwenye umri wa miaka 19, kwa sasa ndiye kinara wa mabao katika Ligi Kuu ya DR Congo (Linafoot), akiwa tayari amefunga mabao 22 msimu huu akiwa na AS Dauphin Noir.

Taarifa kutoka DR Congo zinaeleza kuwa Singida BS imeonyesha nia kubwa ya kumpata mshambuliaji huyo kutokana na kiwango chake bora cha ufungaji, kasi pamoja na uwezo wake wa kucheza ndani na nje ya boksi.

Hata hivyo, timu hiyo ya Tanzania inakabiliwa na ushindani kutoka klabu kadhaa za nje, ikiwemo timu kutoka Ureno ambazo pia zinamfuatilia kwa karibu nyota huyo chipukizi.

Mapendo amekuwa gumzo kubwa kwa timu yake katika Linafoot baada ya kuiongoza safu ya ushambuliaji ya AS Dauphin Noir kwa mafanikio makubwa. Katika michezo kadhaa ya ligi, amekuwa akiibeba timu yake kwa kufunga mabao muhimu, huku baadhi ya vyombo vya habari vya Congo vikimtaja kama mmoja wa washambuliaji bora wanaochipukia kwa sasa nchini humo.

Mbali na kuwa kinara wa mabao, mshambuliaji huyo pia ameweka rekodi ya kipekee kwenye ligi hiyo baada ya kuvunja baadhi ya takwimu zilizowahi kuwekwa na mastaa wa zamani wa soka la Congo akiwemo Trésor Mputu, kutokana na kasi yake ya kufunga mabao akiwa bado na umri mdogo.

Iwapo Singida BS itafanikiwa kukamilisha dili hilo, itakuwa moja ya usajili mkubwa wa klabu hiyo kuelekea msimu ujao.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.