Habari njema kwa mashabiki wa Yanga ni kuwa uongozi wa timu yao umekamilisha mazungumzo ya awali ya kumuongeza mkataba mshambuliaji wake kinara, Prince Dube, katika juhudi za kuhakikisha anaendelea kubaki ndani ya kikosi hicho, imefahamika.
Dube ni miongoni mwa wachezaji muhimu katika kikosi cha Yanga ambao mikataba yao inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu, hali iliyolazimu klabu hiyo kuharakisha mazungumzo ya kumuongezea kandarasi mpya.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya klabu hiyo, pande zote mbili zimefikia makubaliano ya awali na kinachosubiriwa sasa ni hatua ya mwisho ya kusaini mkataba huo rasmi, hatua inayotarajiwa kufanyika muda wowote kuanzia sasa.
Uongozi wa Yanga umeamua kuchukua hatua hiyo baada ya kuridhishwa na kiwango cha mshambuliaji huyo ambaye amekuwa na mchango mkubwa katika safu ya ushambuliaji, akifunga mabao na pia kutoa pasi za mabao muhimu.
Dube kwa sasa ndiye kinara wa mabao ndani ya kikosi cha Yanga SC akiwa amefunga mabao tisa kwenye ligi, sambamba na kutoa pasi nne za mabao, takwimu zinazoonesha mchango wake mkubwa katika mafanikio ya timu hiyo msimu huu.



