Enrique akiri haikuwa rahisi kuitoa Bayern Munich

Joel JJ By Joel JJ • 7th May 2026


Enrique akiri haikuwa rahisi kuitoa Bayern Munich

Kocha mkuu wa Paris Saint-Germain (PSG), Luis Enrique, amesema Bayern Munich ndiyo timu iliyompa wakati mgumu zaidi katika safari yao ya kuelekea fainali ya UEFA Champions League msimu huu.

Enrique ametoa kauli hiyo baada ya PSG kufuzu kucheza fainali kwa kuiondoa Bayern Munich kwa jumla ya mabao 6-5 kufuatia sare ya 1-1 kwenye mchezo wa marudiano uliopigwa Allianz Arena nchini Ujerumani.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Luis Enrique alikiri kuwa Bayern ilikuwa moja ya timu hatari zaidi walizokutana nazo kutokana na ubora wao wa kushambulia na presha kubwa waliyoitoa katika michezo yote miwili ya nusu fainali.

Enrique ameweka wazi kuwa alikuwa akihofia uwezo wa Bayern hasa kutokana na kasi yao ya kushambulia na uzoefu mkubwa waliokuwa nao katika michuano hiyo.

Hata hivyo, kocha huyo amesema hana hofu yoyote kuelekea mchezo wa fainali dhidi ya Arsenal utakaopigwa Budapest mwishoni mwa mwezi huu.

Luis Enrique amesema PSG imeonyesha uwezo mkubwa wa kucheza dhidi ya timu bora Ulaya na ana imani kikosi chake kiko tayari kutetea ubingwa wao wa Ulaya dhidi ya Arsenal.

PSG imefika fainali ya pili mfululizo ya UEFA Champions League baada ya kutwaa taji hilo mwaka 2025 kwa kuichapa Inter Milan mabao 5-0 katika fainali ya kihistoria.

Kwa upande wa Arsenal, timu hiyo imefanikiwa kutinga fainali baada ya kuitoa Atletico Madrid na sasa itakuwa ikisaka taji lake la kwanza kabisa la UEFA Champions League katika historia ya klabu hiyo.

Fainali ya UEFA Champions League 2026 inatarajiwa kupigwa Mei 30 katika dimba la Puskás Aréna mjini Budapest, Hungary, huku PSG ikisaka kuwa timu ya kwanza kutetea taji hilo tangu Real Madrid walivyofanya mwaka 2018.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.