Staa wa kimataifa wa Ufaransa, Kylian Mbappé, anatajwa kuwa katika hali ya sintofahamu ndani ya klabu ya Real Madrid kufuatia taarifa mbalimbali zinazoeleza kuwepo kwa mvutano kati yake na baadhi ya viongozi pamoja na wachezaji wa timu hiyo.
Ripoti kutoka vyombo mbalimbali vya habari vya Ulaya zinaeleza kuwa hali ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo vya Real Madrid si shwari, hasa kuelekea mchezo mkubwa wa El Clasico dhidi ya Barcelona.
Chanzo kikubwa cha mvutano huo kinatajwa kuanza baada ya Mbappe kuonekana kutoridhishwa na maamuzi ya klabu, ikiwemo kuondolewa kwa aliyekuwa kocha Xabi Alonso mapema mwaka huu. Baadhi ya taarifa zinaeleza kuwa nyota huyo alikuwa anaamini kocha huyo alikuwa bado anahitaji kupewa muda zaidi.
Aidha, suala la majeraha yake limeongeza sintofahamu zaidi. Inadaiwa kuwa upande wa Mbappe haukuridhishwa na namna Real Madrid ilivyoshughulikia matibabu yake, huku baadhi ya ripoti zikidai kulikuwa na tofauti za maoni kuhusu muda wa kurejea uwanjani.
Wiki hii pia Mbappe amekuwa akikosolewa na mashabiki wa Real Madrid baada ya kuonekana nchini Italia akiwa kwenye mapumziko mafupi wakati akiendelea kuuguza majeraha. Hatua hiyo imeibua maswali kuhusu kujitolea kwake kwa timu katika kipindi muhimu cha msimu.
Taarifa nyingine zimeeleza kuwa baadhi ya wachezaji ndani ya kikosi hicho hawafurahishwi na kiwango chake cha kujituma hasa katika kusaidia ulinzi, jambo linalodaiwa kuathiri morali ya timu.
Pamoja na hayo yote, kambi ya Mbappe imejitokeza hadharani kupunguza uzito wa taarifa hizo, ikisema baadhi ya habari zinazozungumzwa zimezidishwa na hazionyeshi uhalisia wa kujitolea kwa mchezaji huyo ndani ya Real Madrid.
Hadi sasa, Real Madrid haijatoa tamko rasmi kuhusu madai ya mgogoro huo, lakini taarifa zinazoendelea kutoka Hispania zinaonyesha kuwa kuna hali ya presha kubwa ndani ya klabu hiyo huku msimu ukiwa katika hatua muhimu.
Licha ya changamoto hizo, Mbappe bado anaendelea kuwa mmoja wa nyota muhimu wa Real Madrid baada ya kuonyesha kiwango bora msimu huu kwa kufunga mabao mengi muhimu.



