Paris Saint-Germain wamefanikiwa kutinga fainali ya UEFA Champions League kwa msimu wa pili mfululizo baada ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Bayern Munich na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 6-5. Mchezo huo ulikuwa wa ushindani mkubwa huku Bayern wakijaribu kurejea katika mchezo mbele ya mashabiki wao wa nyumbani, lakini PSG walionyesha utulivu na uzoefu wa mabingwa watetezi.
Ousmane Dembélé aliifungia PSG bao muhimu kwa ustadi mkubwa, kabla ya Harry Kane kusawazisha kwa Bayern kupitia bao la dakika za mwisho lililowapa matumaini mashabiki wa Allianz Arena. Hata hivyo, juhudi hizo hazikutosha kuizuia PSG kufuzu kwenda hatua ya mwisho ya mashindano hayo makubwa barani Ulaya.
Miongoni mwa walioangaza zaidi kwa PSG alikuwa Khvicha Kvaratskhelia, ambaye alitoa kiwango cha juu kwa kutumia kasi, ubunifu na uwezo wake wa kuwatesa mabeki wa Bayern muda wote wa mchezo. Pia Willian Pacho alikuwa imara sana katika safu ya ulinzi, akizuia mashambulizi mengi ya Bayern kwa utulivu mkubwa.
Mchezo huo pia ulikuwa na utata mkubwa baada ya Nuno Mendes kuonekana kugusa mpira kwa mkono akiwa tayari ana kadi ya njano. Mashabiki wa Bayern walidai kadi ya pili, lakini waamuzi waliamua kutoa fauli dhidi ya Konrad Laimer badala yake, pamoja na hilo pia Bayern walilalamikia mpira ulioshikwa na mchezaji wa PSG, Joao neves ikionekana ni penati ya wazi licha ya waamuzi kuamua tofauti na mawazo hayo. Maamuzi hayo yaliibua malalamiko makubwa kutoka kwa upande wa Bayern huku PSG wakivuta pumzi ya afueni.
Sasa fainali ya UEFA Champions League msimu wa 2025/26 imekamilika rasmi, ambapo PSG watachuana na Arsenal FC katika dimba la Puskás Aréna mjini Budapest tarehe 30 Mei 2026. Arsenal wanakuja na ndoto ya kutwaa taji lao la kwanza Ulaya baada ya kusubiri kwa miaka 20, huku PSG wakisaka kuendeleza utawala wao kama mabingwa watetezi.



