Mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Misri zimefikia hatua ya mwisho ya kusisimua zaidi, ambapo mshindi wa msimu wa 2025/2026 ataamuliwa katika siku ya mwisho ya ligi, Mei 20, katika ushindani mkali kati ya Zamalek SC, Pyramids FC na Al Ahly SC.
Huu ni msimu wa kipekee katika historia ya ligi hiyo, ambapo timu tatu zinaingia katika mechi za mwisho zikiwa bado na nafasi ya kutwaa ubingwa, huku mechi zote muhimu zikitarajiwa kuchezwa kwa wakati mmoja.
Zamalek SC wako katika nafasi nzuri zaidi ya kutwaa taji hilo, wana alama 53 wakihitaji pointi moja tu katika mchezo wao dhidi ya Ceramica Cleopatra ili kutangazwa mabingwa wa ligi. Matokeo ya ushindi au sare yatawatosha kumaliza msimu kileleni.
Kwa upande wa Pyramids FC, wao wana alama 51, wanahitaji kushinda dhidi ya Smouha, huku wakisubiri Zamalek wapoteze mchezo wao ili waweze kutwaa ubingwa.
Al Ahly SC, mabingwa wa kihistoria wa soka la Misri, wana alama 50, bado wana nafasi ya kutetea taji hilo, lakini wanahitaji mchanganyiko mgumu zaidi wa matokeo. Wanatakiwa kushinda dhidi ya Al Masry, Zamalek wapoteze, na Pyramids wapate sare ili wao waibuke mabingwa.
Kinachofanya msisimko huo kuwa mkubwa zaidi ni ukweli kwamba mechi zote tatu zitapigwa kwa wakati mmoja, hali itakayowafanya mashabiki kufuatilia matokeo kutoka viwanja tofauti kwa wakati mmoja, huku kila bao likiwa na athari ya moja kwa moja kwenye mbio za ubingwa.
Kuna uwezekano mkubwa Al Ahly msimu huu wakamaliza katika nafasi ya tatu kama timu zote zitashinda mechi zao za mwisho. Ikiwa hivyo Al Ahly watacheza michuano ya kombe la Shirikisho (CAFCC) baada ya misimu mingi ya kutawala ligi ya mabingwa (CAFCL).



