Miamba ya Ulaya, Arsenal FC na Atletico Madrid, leo zinakutana katika mchezo wa mkondo wa pili wa nusu fainali ya UEFA Champions League utakaopigwa katika Uwanja wa Emirates, London.
Timu hizo zinaingia katika mchezo huo zikiwa sare ya bao 1-1 kufuatia matokeo ya mkondo wa kwanza uliochezwa nchini Hispania, hali inayofanya pambano la leo kuwa la wazi kwa kila upande kusaka tiketi ya kutinga fainali.
Arsenal wataingia wakiwa na faida ya kucheza nyumbani, wakitarajia kutumia uungwaji mkono wa mashabiki wao pamoja na rekodi nzuri waliyonayo katika michezo ya nyumbani msimu huu wa michuano ya Ulaya.
Kocha wa Arsenal Mikel Arteta ana matumaini makubwa na kikosi chake, huku nyota wake muhimu wakitarajiwa kuwa fiti kwa ajili ya mchezo huo muhimu.
Kwa upande wa Atletico Madrid, timu hiyo inaingia ikiwa na historia ya kufanya vizuri katika michezo mikubwa ya hatua za mtoano, ikitegemea zaidi nidhamu ya ulinzi na mashambulizi ya kushtukiza.
Kocha wa Atletico Diego Simione anatarajiwa kutumia mbinu zake za kawaida za kujilinda kwa umakini huku akisubiri nafasi za kufanya mashambulizi ya haraka yatakayoweza kuwashtua wenyeji wao.
Wachambuzi wa soka wanasema kuwa mchezo huo unaweza kuamuliwa na tukio moja pekee, kutokana na uwiano wa nguvu kati ya timu hizo mbili.
Kwa mujibu wa utabiri wa awali, Arsenal wana nafasi kubwa kidogo ya kushinda kutokana na faida ya uwanja wa nyumbani, ingawa uwezekano wa mchezo kwenda muda wa ziada au hata mikwaju ya penalti hauwezi kuondolewa.
Mshindi wa mchezo huo atafanikiwa kufuzu kucheza fainali ya UEFA Champions League, ambapo atachuana na mshindi wa mchezo wa pili kati ya Bayern Munich dhidi ya PSG



