Kocha Mkuu wa Yanga Pedro Goncalves amesema kikosi chake leo kinarejea mazoezini kukamilisha maandalizi ya mchezo wa ligi kuu dhidi ya KMC utakaopigwa kesho Jumatano katika uwanja wa KMC Complex.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari mapema leo, Goncalves amesema alitoa mapumziko ya siku moja kwa wachezaji wake baada ya wiki mbili za mfululizo wa mechi.
Kocha huyo raia wa Ureno amesema wanakwenda kuikabili KMC kwa umakini mkubwa lengo lao likiwa kuibuka na ushindi.
"Leo tunarudi kambini kufanya maandalizi ya Mchezo wetu wa kesho dhidi ya KMC, Jana tuliwapa wachezaji Mapumziko baada ya kuwa na wiki mbili kambini ili kujiweka sawa, Tunaamini maandalizi yetu ya leo yatatupa kitu kizuri ili kuhakikisha tunakusanya alama tatu hapo kesho"
Haijalishi tunacheza na nani, lengo letu ni kukusanya alama tatu kwenye kila mchezo, hivyo tutakuwa makini na tutawaheshimu KMC huku tukiingia na malengo yetu ya kushinda mchezo
"Nafahamu kuwa KMC watakuja na Morali kubwa kwasababu wanataka kukusanya alama ili kujiweka sehemu nzuri, watakuja kwa kutuheshimu kwasababu wanacheza na timu inayoongoza ligi, lakini Sisi tutajitoa kwa asilimia mia moja ili kushinda mechi hii," alisema Goncalves.
Yanga ndio vinara wa ligi wakiwa na alama 48 baada ya mechi 20, kimahesabu wanahitaji kushinda angalau mechi 9 kati ya 10 zilizobaki ili kutetea ubingwa kwa msimu wa tano mfululizo.



