Arsenal sasa washindwe wenyewe ubingwa EPL baada ya sare ya Man City

Joel JJ By Joel JJ • 5th May 2026


Arsenal sasa washindwe wenyewe ubingwa EPL baada ya sare ya Man City

Mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England zimechukua sura mpya baada ya Manchester City kulazimishwa sare ya mabao 3-3 na Everton katika mchezo uliopigwa Jumatatu usiku dimba la Goodson Park.

Matokeo hayo yameipa Arsenal faida kubwa kileleni mwa msimamo wa Premier League, huku sasa wakihitaji kushinda mechi zao zilizobaki ili kujihakikishia ubingwa bila kutegemea timu nyingine.

Sare ya maumivu kwa City

Katika mchezo huo wa kusisimua, Everton walionyesha uthubutu mkubwa hasa kipindi cha pili, ambapo Thierno Barry alifunga mabao mawili, huku Jake O'Brien akiongeza bao lingine.

Kwa upande wa Manchester City, Erling Haaland aliendelea kuwa tegemeo kwa kufunga moja ya mabao, kabla ya Jérémy Doku kusawazisha kwa bao la dakika za mwisho kabisa na kuihakikishia timu yake pointi moja muhimu.

Licha ya juhudi hizo, sare hiyo imeonekana kuwa pigo kubwa kwa matumaini ya City kutetea ubingwa wao msimu huu.

Arsenal wanufaika

Matokeo hayo yanaifanya Arsenal kubaki kileleni mwa msimamo kwa tofauti ya pointi tano dhidi ya wapinzani wao wakuu ambao wana mchezo mmoja mkononi. Hali hii ina maana kuwa hatima ya ubingwa sasa iko mikononi mwao wenyewe.

Iwapo Arsenal watafanikiwa kushinda michezo yao iliyosalia, hawatahitaji kuangalia matokeo ya City ili kutwaa taji hilo.

Kauli kutoka kwa kambi ya City

Baada ya mchezo huo, kocha wa City Pep Guardiola alikiri kuwa matokeo hayo yamepunguza kwa kiasi kikubwa nafasi ya timu yake katika mbio za ubingwa, akisisitiza kuwa sasa wanategemea makosa kutoka kwa wapinzani wao.

Presha kwa Arsenal

Hata hivyo, pamoja na kuwa kwenye nafasi nzuri, Arsenal wanakabiliwa na presha kubwa ya kuhakikisha hawatelezi katika hatua za mwisho za msimu. Historia ya ligi hiyo imewahi kushuhudia timu zikishindwa kuhimili presha katika mbio za mwisho.

Kwa mujibu wa ratiba, Arsenal wanakabiliwa na michezo mitatu iliyosalia dhidi ya West Ham United(A), Burnley(H) na Crystal Palace(A).

Manchester City wamebakisha mechi nne dhidi ya Brentford (H), Palace (H), Bournemouth (A) na Aston Villa (H)


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.