Klabu ya Chelsea imeendelea kuporomoka kwenye Premier League baada ya kuchapwa mabao 3-1 na Nottingham Forest katika mchezo uliopigwa kwenye dimba la Stamford Bridge.
Mshambuliaji wa Forest, Taiwo Awoniyi, alikuwa nyota wa mchezo huo baada ya kufunga mabao mawili ya mapema na kuwapa wageni mwanzo mzuri. Awoniyi alifungua pazia la mabao dakika ya 2 kabla ya kurejea tena kufunga bao la tatu dakika ya 52.
Bao jingine la Nottingham Forest lilifungwa na Igor Jesus kwa njia ya mkwaju wa penalti dakika ya 15, baada ya safu ya ulinzi ya Chelsea kufanya makosa yaliyoigharimu timu hiyo.
Chelsea walipata bao lao pekee mwishoni mwa mchezo kupitia João Pedro, lakini halikutosha kuokoa jahazi lao lililokuwa tayari limezama.
Licha ya kupata nafasi kadhaa, ikiwemo penalti, Chelsea walishindwa kuitumia ipasavyo, jambo lililozidi kuongeza presha kwa benchi la ufundi na wachezaji wake.
Matokeo hayo yanaifanya Chelsea kuendelea kuyumba katika msimamo wa ligi, huku Nottingham Forest wakijiongezea matumaini ya kubaki salama katika ligi hiyo baada ya ushindi muhimu ugenini.



