Kocha Mkuu wa Simba SC Steve Barker, amesema matumaini ya ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara yameanza kuyumba baada ya timu yake kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Yanga katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.
Simba ilianza mchezo kwa kasi na kufanikiwa kupata mabao mawili ya mapema kupitia kwa Libasse Gueye na Clatous Chama, lakini kupoteza umakini na kupungua kwa kasi kuliiwezesha Yanga kurudi mchezoni na kusawazisha kupitia kwa Prince Dube na Bakari Nondo Mwamnyeto, hali iliyosababisha pointi kugawanywa.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Barker alikiri kuwa matokeo hayo siyo waliyoyatarajia katika mbio za ubingwa.
“Hatukufurahishwa na matokeo ya mchezo huu kwani tulifahamu tunapaswa kushinda ili kuendeleza presha kwenye mbio za ubingwa,” alisema.
Aliongeza kuwa Simba ilianza vyema lakini ilishindwa kuendeleza kasi hiyo.
“Tulianza vyema mchezo na kufunga mabao mawili ya haraka. Tulipunguza kasi baada ya bao la pili,” alisema.
Barker alisema kuwa kuruhusu Yanga kurudi mchezoni kulitokana na kushuka kwa presha ya ushambuliaji kwa upande wa Simba.
“Nafikiri tulipaswa kuendeleza presha tuliyoanza nayo. Walipofunga bao la kwanza waliongeza kujiamini na sisi tukaanza kucheza na presha ndogo,” alieleza.
Katika kipindi cha pili, kocha huyo alisema mchezo ulifunguka zaidi na kila timu ilipata nafasi za kufunga, hali iliyochangia matokeo hayo.
“Kipindi cha pili baada ya bao la pili, mchezo ukawa wazi zaidi. Kila timu ilikuwa hatari kwenye mashambulizi ya kujibu,” alisema.
Hata hivyo, Barker alikiri kuwa kwa mashabiki mchezo ulikuwa wa kuvutia kutokana na mabao manne kufungwa, lakini kwa upande wa Simba ulikuwa ni upotevu wa nafasi muhimu.
“Kwa mashabiki waliotazama mpira ni wazi wamefurahia burudani, lakini kwetu si matokeo tuliyohitaji,” alisema.
Kocha huyo alisisitiza kuwa bado kuna mechi nyingi zilizobaki na Simba italazimika kushinda zote ili kuendeleza matumaini ya ubingwa.
“Bado kuna mechi nyingi. Tunapaswa kushinda kila mchezo ili kuendelea kuwapa presha wapinzani wetu. Mbio za ubingwa bado hazijaisha,” aliongeza Barker.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga iendelee kutamba kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama tano ikiwa na alama 48 huku Simba inayoshika nafasi ya pili ikiwa na alama 43 baada ya timu zote kucheza mechi 20.
Ni wazi mechi 10 za mwisho kuhitimisha msimu zitakuwa na ushindani mkali, Yanga wakiwa na nafasi kubwa ya kutetea taji lao kama watafanya vizuri katika mechi hizo.



