Barcelona kutangaza ubingwa El Classico?

Joel JJ By Joel JJ • 3rd May 2026


Barcelona kutangaza ubingwa El Classico?

Klabu ya FC Barcelona imepiga hatua kubwa kuelekea ubingwa wa La Liga kufuatia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya CA Osasuna katika mchezo uliochezwa Uwanja wa El Sadar Jumamosi usiku.

Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkali, Barcelona walilazimika kusubiri hadi dakika za mwisho kuvunja ukuta wa Osasuna waliocheza kwa nidhamu kubwa mbele ya mashabiki wao.

Mshambuliaji wa Barcelona, Robert Lewandowski, aliifungia timu yake bao la kwanza dakika ya 81 kwa mpira wa kichwa uliotokana na krosi ya upande wa kulia. Dakika chache baadaye, Ferran Torres aliongeza bao la pili, akiipa Barcelona uongozi wa mabao mawili.

Osasuna walijibu haraka kupitia Raúl García aliyefunga bao la kufutia machozi dakika ya 88, lakini haikutosha kuzuia ushindi wa wageni hao.

Ushindi huo unaifanya Barcelona kuendelea kuongoza msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama 14 dhidi ya mahasimu wao wakuu, Real Madrid CF, huku mbio za ubingwa zikikaribia kufikia tamati.

Matokeo hayo yanaongeza uwezekano wa Barcelona kutangazwa mabingwa katika mchezo wao ujao dhidi ya Real Madrid maarufu kama El Clásico, au mapema kama wapinzani wao Real Madrid watapoteza mchezo dhidi ya Espanyol leo.

Kocha wa Barcelona, Hansi Flick, alisema baada ya mchezo huo kuwa timu yake imeonyesha uvumilivu na nidhamu katika dakika muhimu, akisisitiza kuwa bado wanahitaji kumalizia kazi katika michezo iliyosalia.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.